Mpango wa kunusuru kaya masikini Tasaf umedhamiria kuhamasisha uanzishwaji wa vikundi vya kuweka akiba vya walengwa ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha walengwa wanakutana kwa pamoja na kubadilishana mbinu za kujikwamua kiuchumi na kusaidiika kirahisi
Hayo yamebainishwa na mratibu wa Tasaf wa halmashauri ya manispaa Ilemela ndugu Frank Ngitaoh wakati wa utekelezaji wa zoezi la kunusuru kaya masikini dirisha la Machi-Aprili kwa awamu ya Kumi na moja ikijumuisha mitaa Sitini na tisa inayonufaika na mpango huo ya kata Kumi na nane isipokuwa kata ya Kahama ambapo kaya Elfu Nne mia nne na sita zitalipwa zaidi ya milioni mia moja na thelathini na sita
Ngitaoh ameongeza kuwa zoezi hilo litatanguliwa na shughuli za kuboresha taarifa za walengwa kwa kuongeza taarifa za watoto na walioko shuleni kwa chini ya miaka mitano ambao hawakuorodheshwa katika kipindi cha usajili wa awali, kusomewa rasimu ya walengwa wahitimu kwenye mpango na kukusanya taarifa ya walioondolewa kwa kutojitokeza kuchukua malipo yao kwa zaidi ya mara tatu mfululizo
‘… Awamu hii tumedhamiria kuhamasisha uanzishwaji wa vikundi vya walengwa wa mpango huu ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha walengwa wanakutana kwa pamoja na kubadilishana mbinu mbalimbali za kujikwamua kiuchumi na kusaidiika kirahisi kutoka serikalini …’ alisisitiza
Kwa upande wake mwenyekiti wa uhamasishaji wa mpango kutoka mtaa wa Kigala uliopo kata ya Buswelu Bi Aisha Abubakar amesema kuwa muitikio wa zoezi hilo kwa sasa umezidi kuwa mzuri ukilinganisha na hapo awali ambapo utaratibu wa kupiga vipenga ulikuwa ukidumaza ubora wa zoezi hilo ukilinganisha na sasa ambapo wanufaika wanafuatwa kaya kwa kaya kuelimishwa mambo muhimu ya mradi
Aidha wanufaika wa mradi akiwemo Bwana Edward Masanyiwa kutoka mtaa Kigala ameishukuru serikali kwa utaratibu wa mpango huu wa kunusuru kaya masikini ambapo wanufaika wamekuwa wakitumia fedha wanazopata kuanzisha miradi mbalimbali ya kilimo,uvuvi, ufugaji na biashara ndogo ndogo kunakowafanya waache utegemezi na kujikwamua kiuchumi
Akihitimisha mwenyekiti wa mtaa Kigala ndugu Hamisi Magawila amesema kuwa pamoja na jitihada zote zinazochukuliwa ameiomba serikali kuzidi kutoa elimu kabla ya utekelzaji wa mpango ili wananchi waweze kupata uelewa wakutosha juu ya mpango kwani wengi wao wamekuwa wakipoteza haki zao za msingi kwa kutofahamu utaratibu ikiwemo kutotoa taarifa za watoto wadogo na wanafunzi
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.