Timu kutoka makao makuu ya TASAF - Dodoma ikiongozwa na Mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano TASAF Bi.Zuhura Mchungi imeanza ziara yake ya siku tatu kutembelea miradi inayofadhiliwa na OPEC na kutekelezwa na mradi wa kupunguza kaya maskini - TASAF katika Manispaa ya Ilemela.
Ugeni huo umetembelea jumla ya miradi 12 inayotekelezwa katika shule ya sekondari Igogwe iliyopo kata ya Bugogwa ambayo ni ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa,matundu 12 ya vyoo, maabara 2 za sayansi, ujenzi wa jengo la utawala na ujenzi wa hosteli ya wasichana.
Akitoa ufafanuzi wa gharama iliyotumika katika miradi hiyo Mratibu wa TASAF Manispaa ya Ilemela Leonard Nyamgenda Robert amesema jumla ya kiasi cha shilingi milioni 863.2 ilipokelewa na mpaka sasa kiasi cha shilingi milioni 516.3 imetumika na kazi ya ukamilishaji inaendelea.
Nae mwakilishi wa Mkuu wa shule ya sekondari Igogwe Mwl.Innocent Bundu Mashauri amekiri kuwa kukamilika kwa miundo mbinu hiyo kutasaidia kuongeza ufaulu kwa wanafunzi kutokana na uwepo wa mazingira rafiki kwa waalimu na wanafunzi,imepunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu karibu km 7 kufuata huduma ya shule sambamba na kutokomeza changamoto ya mimba mashuleni kwa wanafunzi wa kike.
" Hongereni sana Ilemela kwa mradi huu ambao jamii imekiri kushirikishwa kikamilifu,kazi iliyofanyika ni kubwa na inaonekana.Natoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo tuungane kuhakikisha watoto wetu wanasoma katika mazingira mazuri." Amesema Bi.Zuhura Mchungi
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.