Timu ya wataalam kutoka mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF) makao makuu ikiongozwa na mjumbe wa bodi ya TASAF taifa Dkt.Naftal Bernad Ng’ondi na kaimu Mkurugenzi wa TASAF Oscar Maduhu imetembelea baadhi ya miradi kuona utekelezaji wake,kufahamu changamoto na kutoa ushauri na mapendekezo katika kuboresha na kuongeza ufanisi kwa wasimamizi wa miradi hiyo.
Akitoa taarifa juu ya utekelezaji wa miradi mbalimbali Mratibu wa TASAF Manispaa ya Ilemela Leonard Robert amesema jumla ya Bilioni 1.2Tshs. imetumika kwa ajili ya ujenzi na maboresho ya miundo mbinu ya elimu sekondari huku elimu msingi ikigharimu Milioni 336.7Tshs. sambamba na miradi ya afya iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 323.8 kuanzia mwaka 2021 hadi 2023.
“…Mradi wa shule ya mfano ya sekondari Igogwe ulipokea kiasi cha shilingi milioni 868.1Tshs kwa ajili ya miundo mbinu wezeshi 12 ikiwemo vyumba vya madarasa vinne,matundu 12 ya vyoo, maktaba, maabara, mabweni ya wavulana na wasichana, jengo la utawala sambamba na manunuzi ya samani mbalimbali…”
Dkt.Ng’ondi ametoa pongezi nyingi kwa uongozi mzima wa Ilemela kwa kazi nzuri ya ujenzi iliyokamilika na nyingine inayoendelea na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za kuleta maendeleo zaidi ndani ya Manispaa ya Ilemela.
“Natambua jitihada za Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha miundo mbinu mbalimbali ndani ya sekta ya elimu na afya kwa kuona umuhimu mkubwa,huu ni mradi maalum ni lazima ulindwe ili tupate matokeo chanya yaliyokusudiwa”
Nae Kaimu Mkurugenzi wa TASAF Oscar Maduhu amesema miundo mbinu mizuri ni chachu ya wanafunzi kupenda kusoma na kuongeza ufaulu.
“Mbali ya mradi wa uhawilishaji fedha kwa walengwa wa kaya maskini,tutaendelea kujenga na kuboresha miradi mbalimbali ya kijamii kuleta unafuu wa maisha kwa wananchi wetu.”
Athanas Manyika ni Mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Igogwe yeye anatoa shukrani nyingi kwa serikali huku akikiri kuwa uwepo wa miradi ya TASAF shuleni kwake umewapa heshima na kurahisisha utendaji kazi kwa waalimu na wanafunzi kuwa na ari ya kupenda kusoma kwa bidii zaidi kutokana na mazingira rafiki yaliyopo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.