Mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF umelenga kuanzisha miradi ya maendeleo itakayosimamiwa na kutekelezwa na kaya za walengwa walioandikishwa katika mpango huo kwa ngazi za mitaa kwa lengo la kuwaongezea ujuzi, ajira na kuboresha miundombinu yao
Hayo yamesemwa na mratibu wa mpango huo katika manispaa ya Ilemela Ndugu Leonard Robert Nyamgenda wakati wa zoezi la uhawilishaji fedha kwa dirisha la malipo la mwezi Mei-Juni 2024 ambapo amesema kuwa walengwa watajengewa uwezo kwaajili ya kuanzisha miradi katika maeneo yao watakayokuwa na uwezo wa kuitekeleza kwa nguvu zao wenyewe na si kwa kutumia mashine au wakandarasi
“Walengwa watafanya kazi katika miradi midogomidogo kama ujenzi wa barabara, visima na mingine watakayoona wao inafaa katika mtaa wao kwa kutumia nguvu kazi zao wenyewe kwa siku kumi kwa mwezi, kwa masaa yasiyozidi matatu na kwa ujira wa shilingi elfu tatu”, Alisema
Deograsia Lubugo ni mwezeshaji wa mpango wa kunusuru kaya masikini kata ya Nyakato ambapo amesema kuwa licha ya miradi hiyo kutekelezwa na wanufaika wa mpango wa TASAF lakini pia miradi ikishakamilika itabaki kuwa mali ya jamii nzima na kwamba zipo faida nyingi zitakazopatikana kupitia uanzishwaji wa miradi ikiwemo kukuwa kwa miundombinu, ajira na kujipatia kipato.
Nae mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kangaye ‘B’ Joseph Nyabinyiri akaongeza kuwa utaratibu wa uanzishaji wa miradi kwa walengwa utawasaidia walengwa kujiongezea
kipato cha ziada tofauti na kile kinachopatikana moja kwa moja kupitia mpango sanjari na kuwafanya kuwa na nidhamu zaidi ya fedha kwani sasa watakuwa wakipata kipato kwa kufanya kazi badala ya ile inayotolewa bila kufanya kazi yeyote pamoja na kuleta maendeleo ya pamoja katika mtaa kupitia miradi itakayotekelezwa.
Bi Rahel Shimba na Bi Nyakaho Mgaya Malemba ni wanufaika wa mpango kutoka mitaa ya majengo mapya kata ya Nyakato ambapo wameipongeza na kuishukuru serikali kuja na mpango huo kwani utasaidia kutatua kero ya ubovu wa barabara katika mtaa wao na kwamba utasaidia kutatua kero zilizo katika jamii katika maeneo mengine kulingana na uhitaji bila kutumia gharama kubwa na muda mrefu kwa kuwa kazi hizo zitakuwa zikifanywa na wanufaika wa mtaa husika.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.