SHULE YA DERBY GRAMMAR KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA MANISPAA YA ILEMELA
Shule ya Derby Grammar kutoka nchini Uingereza yenye mahusiano ya kirafiki na shule ya msingi Ibeshi ya Manispaa Ilemela mkoani Mwanza imesema kuwa itaendelea kuimarisha uhusiano wake na Ilemela kuhakikisha wanamaliza changamoto mbalimbali za sekta ya elimu.
Akizungumza kwa niaba ya ugeni huo Kaimu Mkuu wa shule ya Derby Grammar Bi Lesley Reynolds amesema kuwa mahusiano ya shule yake na shule ya Ibeshi ni kwa manufaa ya pande zote mbili katika kupunguza changamoto mbalimbali za elimu walizonazo watu wao na kuongeza kuwa ujio wao ni wa awamu na mara zote umekuwa ukija na mpango mkakati wa kupunguza changamoto walizonazo
“Yapo tuliyoyafanya kwa awamu iliyopita lakini kwa sasa tumejitahidi kujenga darasa, kutoa madawati 30, kuweka umeme,kununua madaftari na kalamu 10 kwa kila mtoto kwa watoto 1286, kupaka rangi na tumefundisha masomo ya hesabu kiingereza michezo na mambo ya jinsia lengo ni kupunguza changamoto wanazokutana nazo watu wetu kutoka pale tulipoishia awamu ya kwanza”, Alisema, Aidha ameongeza kuwa katika kuimarisha afya za wanafunzi kupitia michezo wametoa jumla ya shilingi Milioni Tano kwaajili ya kusawazisha uwanja wa Michezo wa shule hiyo ili kufikia lengo walilolikusudia.
Nae Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Ndugu John Wanga pamoja na Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mheshimiwa Renatus Mulunga mbali na kushukuru ugeni huo kwa kuendelea kushirikiana na manispaa ya Ilemela katika kutatua changamoto mbalimbali za elimu hasa zinazoikabili shule ya msingi Ibeshi, ameahidi kuendeleza uhusiano huo sambamba na kuomba uwepo wa mpango wa kubadilishana wataalamu ili kuongeza ufanisi wa shughuli tofauti tofauti zinazofanywa.
“Niwaahidi tu mahusiano haya tutayaendeleza na ninaamini katika kipindi kijacho tungeanzisha utaratibu wa kubadilishana wataalamu kujiongezea uwezo zaidi hili hatulilazimishi ila nadhani ingekuwa vizuri sana”, Alihitimisha Mkurugenzi huyo
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.