Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kupitia Idara ya maendeleo ya jamii Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 imefanikiwa kutoa jumla ya Shilingi 501,000,000(Shilingi Milioni mia tano na moja tu) kwa vikundi 186 vya wanawake, vijana na walemavu.
Kati ya vikundi hivyo, vikundi 148 vya wanawake vimepatiwa kiasi cha Tsh 397,000,000, vikundi vya vijana 33 vimepatiwa jumla ya Shilingi 92,000,000 na vikundi 5 vya walemavu vimepatiwa jumla ya Shilingi 12,000,000.
Jumla ya fedha iliyo rejeshwa hadi sasa ni takribani kiasi cha Shilingi 62,000,000 huku pesa zingine zikiendelea kurejeshwa kulingana na mkataba wa marejesho wa fedha hizo.
Kikundi cha Masaligula ni mojawapo ya kikundi kinachofaidika na mkopo huu kutoka Halmashauri kilichopo Kata ya Sangabuye na hujishughulisha na shughuli ya mradi wa uuzaji wa dagaa pamoja na mgahawa.
Mhasibu wa kikundi hicho Bibi Elizabeth Bahati amesema kuwa hii ni mara ya pili kikundi chao kinapata mkopo huu ambapo awamu ya kwanza walipata fedha kiasi cha Shilingi Milioni mbili na awamu ya pili wamepata mkopo wa Shilingi Milioni tatu.
Aidha aliongeza kwa kusema kuwa, mkopo huu umewasaidia kukuza biashara yao kwani hapo awali alikuwa wakilangua dagaa na kutembeza kwenye mabeseni lakini kwa sasa wanaweza kununua dagaa kwenye magunia toka kwa wavuvi na uwauzia wanaotembeza kwenye mabeseni.Aliongeza kuwa mafanikio mengine yaliyopatikana kutokana na mkopo huu, ni kuwa wameweza kuwasomesha watoto kupitia fedha wanazopata kupitia biashara hiyo.
Pia amewashauri wakinamama kujinga na vikundi mbalimbali ili waweze kupata mkopo huo kwani hauna riba na ni wenye masharti nafuu huku akiwaasa wale ambao wamekuwa hawarejeshi mkopo kuhakikisha wanarejesha kwa wakati ili kujenga uaminifu.
Pamoja na hayo kwa niaba ya wanufaika wa mkopo huo,Bi Elizabeth ameishukuru serikali kwa kuanzisha utaratibu huo wa utoaji wa mkopo usiokuwa na riba kwani umewarahisishia maisha na kuwaletea maendeleo.
Fedha hii inayokopeshwa kwa wanawake,vijana na walemavu ni asilimia 10 ya fedha kutoka makusanyo ya ndani ya halmashauri na hukopeshwa kwa muda wa mwaka mmoja bila riba ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala ya mwaka 2015-2020.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.