Zaidi ya shilingi milioni 34 za kitanzania zimetolewa na serikali kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF
Akizungumza wakati wa zoezi la udumbukizaji wa vifaranga vya Samaki katika eneo la ufugaji, mratibu wa TASAF manispaa ya Ilemela Ndugu Leonard Robert amefafanua kuwa mradi huo unahusisha vizimba viwili vyenye jumla ya Samaki elfu kumi na tatu utakaotekelezwa na walengwa wa TASAF.
‘... Tutakeleza mradi wa ufugaji samaki katika vizimba vilivyopo Kamanga Sengerema, Kikundi cha walengwa kilichochaguliwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu ni kutoka Kayenze ndogo, Ni matarajio yetu mradi huu utaenda kunufaisha walengwa waliokusudiwa ...’ alisema
Aidha mratibu Leonard amewataka walengwa wanaonufaika na mradi huo kuhakikisha wanausimamia vizuri na kuthamini thamani ya fedha iliyowekezwa katika mradi huo ili tija iliyokusudiwa iweze kupatikana
Paschal Peter Mgalu ni afisa uvuvi manispaa ya Ilemela ambapo amefafanua kuwa idara ya uvuvi ya manispaa hiyo itahakikisha inashirikiana na walengwa hao kwa kuwasaidia ushauri na msaada wa kitaalam kila itakapohitajika ili kuhakikisha mradi huo unastawi pamoja na kufikia lengo lililokusudiwa la kupunguza masikini kwa wananchi
Kwa upande wake Bi Modesta Chigugu ambae ni mlengwa wa TASAF na kiongozi wa kikundi cha wanufaika na mradi huo akasema kuwa ana matumaini makubwa na mradi huo katika kuwapunguzia umasikini sanjari na kuahidi kuusimamia vizuri ili waweze kuondokana na umasikini
Nae Bi Lutigayi Basililo ambe ni msimamizi wa mradi huo (CMC) akaongeza kuwa wamepokea mradi huo kwa furaha kubwa sambamba na kuhakikisha wanahamasishana kufanya kazi kwa bidii ili mradi huo usife
Bwana Mkapa Zacharia ambae ni meneja msaidizi wa kampuni ya SIR MECK LTD na mtaalam wa ukuzaji wa viumbe maji akasema kuwa kampuni yake imeingia mkataba na manispaa ya Ilemela kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF kwaajili ya kuwauzia vifaranga, chakula cha Samaki, kuhudumia samaki hao, kuwavuna na kisha kuwatafutia soko
Mradi wa vizimba kwa ajili ya ufugaji wa Samaki katika Ziwa Viktoria manispaa ya Ilemela kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF manispaa ya Ilemela utatekelezwa kwa muda wa miezi tisa.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.