Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe Amir Mkalipa amekabidhi mbegu za mahindi kilo 168 sambamba na mbolea mifuko 42 zenye thamani ya Shilingi takriban milioni 5 fedha za mapato ya ndani kwa wakuu wa shule za sekondari 9 na shule za msingi 21.
Mhe Mkalipa alibainisha lengo la kukabidhi mbegu hizo, ni kuhakikisha watoto wanapata chakula mashuleni, "kwanza tutakuwa tumekidhi kigezo cha lishe mashuleni lakini tutakuwa tumechangia mchango mkubwa hasa kwa wazazi wasiotoa chakula",alisema
"Maelekezo yangu kwenu maafisa elimu shamba la shule halimi mzazi analima mwanafunzi na hiyo ni sehemu ya stadi zao za kazi za kila siku, kwahiyo wasimamieni wanafunzi walime maeneo yao kwa ajili ya chakula chao", alisisitiza Mhe Mkalipa
Aidha Mhe Mkalipa aliongeza kusema kuwa iwapo mashamba yatakufa, maafisa ugani watawajibika kwasababu utakuwa hajawajibika hivyo wanapaswa kusimamia suala hili la kilimo mashuleni ili kuwezesha upatikanaji wa chakula mashuleni.
Nae Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Bi Ummy Wayayu, akimshukuru Mhe Mkalipa kwa kuleta wazo hili la kuanzisha mashamba shuleni, alisema kuwa ana imani kuwa maeneo haya yakisimamiwa vizuri kitapatikana chakula cha kutosha na wanafunzi watapata chakula mashuleni ambacho kitawapelekea wao kusoma vizuri na kufanya vizuri katika masomo yao.
Grace Minja ni afisa kilimo kata ya kiseke , kwa niaba ya maafisa kilimo wote ameushukuru uongozi wa wilaya ya Ilemela kwa kuwapatia mbegu kwa ajili ya kupanda mashuleni kwa lengo la kuboresha lishe mashuleni na kuongeza ujuzi na ustadi wa wanafunzi huku akiahidi kufanyia kazi maelekezo yote ili kupata mavuno yenye tija
Nae Mwl Ibrahim Mwakatobe kutoka shule ya msingi Igogwe, amesema kuwa wataendelea kusimamia suala zima la kilimo mashuleni kama maelekezo ya Mkuu wa Wilaya yanavyosema ili kuweza kupata mazao kama lengo lililokusudiwa


Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.