"Endeleeni kutoa huduma ya kuwatumikia watanzania, endeleeni kutunza rasilimali na miundombinu ya afya , pamoja na dawa zinazokuja"
Ni kauli ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe Amir Mkalipa wakati akifunga kikao kazi cha tathmini ya utendaji kazi wa idara ya afya katika kipindi cha miezi sita siku ya jumatano ya tarehe 22 oktoba 2025.
Aidha Mhe Mkalipa, aliwapongeza idara ya afya kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya kwani hajapokea malalamiko kutoka kwa wananchi hivyo ni tafsiri ya kuwa wanatimiza wajibu wao wa msingi
"Sisi tumewapeni imani yetu, ninajua imani yetu tuliyowapa mtaenda kutulipa kwa kuwatumikia wananchi wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye kipande tulichopewa cha wilaya ya Ilemela", Alisema Mhe Mkalipa
Nae Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Bi Ummy Wayayu, pamoja na kuwapongeza kwa kazi kubwa ambayo idara ya afya imekuwa ikiifanya ya kuwahudumia wananchi, amemuahidi Mkuu wa Wilaya kuwa atahakikisha vituo vyote vya kutolea huduma za afya vinatumia mfumo wa GotHOMIS katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya vituo hivyo.
"Nitahakikisha nasimamia vituo vyote vinakusanya kwa kutumia mfumo wa GoTHOMIS, kwani kuna faida kubwa ya kutumia mifumo kwani tunaongeza fedha za makusanyo ambayo mwisho wa siku yana faida kubwa katika vituo vya afya na zahanati ambapo wataweza kuendesha shughuli zao kupitia mapato hayo kuliko kutegemea fedha za wadau", Alisema Mkurugenzi Ummy
Akibainisha lengo la kikao kazi hicho, mganga mkuu wa Manispaa ya Ilemela, Bi Maria Kapinga alisema kuwa lengo ilikuwa ni kufanya tathmini ya utendaji kazi wa idara ya afya wa miezi 6 kwa kipindi cha kuanzia mwezi April hadi Sept 2025 ili kuendelea kuboreshaji wa huduma za afya ndani ya manispaa ya Ilemela, sambamba na kuwatambua viongozi bora, vituo vilivyofanya vizuri katika Basket Fund, vituo vilivyofanya vizuri katika huduma za chanjo vituo vilivyofanya vizuri katika usimamizi wa mapato kwa kuwapatia vyeti vya pongezi.
Kikao hicho kilihusisha timu ya usimamizi wa huduma za Afya (CHMT), waganga wafawidhi wa vituo, matron na patron wa vituo, makatibu wa afya na wahasibu wa vituo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.