Serikali itaendelea na juhudi za kuwatunza na kuwalea watoto kwa kutunga sheria zinazolinda watoto, kuanzisha wizara inayosimamia watoto, kutekeleza miradi inayonufaisha watoto pamoja na kutoa fursa ya ushiriki wa wadau katika kuhudumia watoto
Hayo yamebainishwa na Katibu tawala wa wilaya ya Ilemela Wakili Bi Mariam Abubakar Msengi wakati akifungua kikao kwa kundi la watu wa kuaminika kutoka manispaa ya Ilemela katika ukumbi wa hoteli ya Golden Pegion kwa ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la Railway Children ambapo amesema kuwa ipo sheria namba 21 ya mwaka 2009 iliyotungwa na itakayoendelea kusimamiwa kwa lengo la kusaidia watoto na kutoa fursa ya kutunza watoto kupitia watu wa kuaminika
'.. Serikali ya jemedari wetu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka juhudi katika kutunza na kulea watoto, Fedha nyingi zimetolewa kutekeleza miradi yenye manufaa ya moja kwa moja kwa watoto, Ilemela tumejenga madarasa kwaajili ya watoto wetu, tumejenga bweni la watoto wenye mahitaji maalum ..' Alisema
Aidha Wakili Bi Msengi ameipongeza taasisi ya shirika la Railway Children kwa namna wanavyojitoa na kutekeleza miradi mbalimbali yenye kulenga watoto na kuwaunga mkono watu wakuaminika kwa kuwapa mafunzo na vifaa ili kuwarahisishia utekelezaji wa majukumu yao pamoja na kuwaahidi ushirikiano katika kufanikisha shughuli zao za kila siku
Kwa upande wake meneja mradi huo kutoka shirika la Railway Children Bi Irene Wampembe amefafanua kuwa wao kama shirika wameamua kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha huduma za malezi na matunzo ya watoto kwa kugawa magodoro, neti na mashuka kwa watu wa kuaminika ili kuwarahisishia utoaji huduma kwa watoto wanaowalea pamoja na kuishukuru wilaya ya Ilemela kwa ushirikiano inaowapa huku wakiahidi kuendelea na utatuzi wa kero na changamoto za wananchi kupitia utekelezaji wa miradi ya taasisi hiyo
Pamela kijazi ni afisa ustawi wa manispaa ya Ilemela ambapo amefafanua kuwa mafunzo hayo yamehusisha watu wa kuaminika 23 kutoka kata za manispaa ya Ilemela na wengine 8 kutoka kituo cha stendi ya Nyamhongolo .
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.