Kaimu Mkurugenzi wa hospitali ya rufaa ya Bugando Dkt. Cosmas Mbulwa ametoa elimu kwa wanawake wa Ilemela waliojitokeza kutembelea wodi ya kansa na kutoa msaada wa mahitaji ikiwa ni miongoni mwa shughuli walizojipangia kufanya kuelekea siku ya wanawake duniani
Akizungumza na kina mama hao wa kutoka wilaya ya Ilemela Dkt.Cosmas amesema saratani ni mgawanyiko wa seli kwenye kiungo chochote mwilini bila mpangilio unaopelekea kutokea kwa uvimbe mkubwa ambao mwanzoni hauna maumivu yoyote.
Amewataka wanawake hao kuwa na utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara ili kujua hali zao kwani ugunduzi wa ugonjwa huo mapema inaweza kurahisisha matibabu yake katika hatua za awali huduma inayotolewa bure katika hospitali zote za serikali.
“.. Mpaka sasa bado hakuna tiba ya saratani,tafiti bado zinaendelea. Pendeni kutumia matunda mbalimbali hasa stafeli na mazao ya mti wake kwa sababu watafiti wengi wamekuwa wakisema linasaidia kuimarisha seli za mwili katika kupambana na maradhi japo hawajasema wazi vipimo halisi vya matumizi mstafeli ..”
Akitaja vitu vinavyohisiwa kuwa vichocheo vya maradhi hayo na vinavyoweza kuepukika amesema uvutaji wa sigara,uvutaji shisha,uvutaji bangi ,unywaji pombe uliokithiri sambamba lishe mbaya isiyo na uwiano sahihi wa kiasi na mchanganyiko wa chakula,vingine ni pamoja na kuwa na uzito mkubwa.
Mkurugenzi wa shirika la Hope for youth development organization (HYDO) Bi. Anitha Dotto amesema elimu hiyo ya saratani iliyotolewa imekuwa msaada mkubwa kwao na kwamba jamii nzima bado inahitaji kujua zaidi kuhusu ugonjwa huo .
“..tumeambiwa ni ugonjwa ambao unahusisha vinasaba ,mtindo wa maisha kwa kweli jamii hasa za pembezoni zinahitaji kupelekewa elimu hii sana ,ni vigumu kwa mwananchi wa kawaida kufahamu hivi vitu..”
Vitu vilivyotolewa katika wodi hiyo ya wagonjwa wa kansa ni pamoja na pesa taslim shilingi laki 4 na mahitaji ya muhimu kama pampasi za watoto na watu wazima,smafuta ya kujipaka,dawa za meno ,ndala,miswaki,sabuni za unga na vipande ,sabuni za maji ,vyakula kama mchele ,maziwa ya unga, sukari na juisi.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.