Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Said Mtanda leo Machi 17,2025 amewatembelea wafanyabiashara wa mbao eneo la Sabasaba wilayani Ilemela waliopatwa na ajali ya moto na kuwapa pole na kuwaomba kuwa na utulivu wakati taarifa ya uchunguzi wa chanzo cha moto huo ikiendelea kufanyika.
Akizungumza nao mara baada ya kutembelea maeneo yaliyoathirika na moto huo,mkuu huyo wa mkoa amesema mara baada ya taarifa hiyo kukamilika na kusomwa, Ofisi yake itakutana na wafanyabiashara hao pamoja na taasisi za fedha ili kuona namna ya kuwapa muda zaidi wa marejesho ya fedha kwa wale waliokopa.
"Natoa rai kwa vyombo vya dola kuharakisha uchunguzi huu ili kutambua chanzo na kujua nini kifanyike na wafanyabiashara hao waendelee na shughuli zao mapema iwezekanavyo kama Serikali inavyohimiza wananchi kuwajibika",Mtanda
Aidha amewataka wafanyabiashara hao kuzingatia matumizi ya vifaa vya kuzimia moto na bima ambayo itawasaidia kuepuka hasara kubwa yanapotokea majanga ya moto kama hilo.
Amebainisha mara baada ya kutembelea maeneo yaliyoathirika na moto huo amepata taarifa idadi kubwa hawatumii vifaa vya kuzimia moto licha ya elimu ya matumizi hayo kutolewa mara kwa mara na Jeshi la zimamoto na uokoaji.
"Serikali kuna maeneo ya majanga inawajibika moja kwa moja kuwagharamia wananchi na mengine haiwajibiki nayo kama hili,narudia kuwakumbusha kuzingatia sheria zinavyotaka ili kujihakikishia usalama wa muda wote wa mali zenu,niwapongeze pia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kufanya kazi hii kwa weledi na kuokoa sehemu kubwa ya mali za wafanyabiashara hawa,"mkuu wa mkoa
Kwa upande wake kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza SSF Elisa Kamugisha amebainisha moto huo ulianza majira ya saa saba usiku na kufanikiwa kwa asilimia kubwa kuwahi kuuzima usienee sehemu nyingine.
"Hapa kuna wafanyabiashara wa mbao zaidi ya elfu moja lakini walioathirika na janga la moto ni thelasini,lakini taarifa rasmi itatolewa muda siyo mrefu", SSF Kamugisha.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.