Watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wametakiwa kuhakikisha wanatimizia wajibu wao kwa kuwa waadilifu na kuwatendea haki wananchi kwani kazi ni ibada na ni msingi wa utu.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa lengo la kujitambulisha kwao, kutoa uelekeo wa utendaji kazi sambamba na kuwakumbusha wajibu wa watumishi wa umma na kuboresha masuala ya ushirikiano, uhusiano na mawasiliano kazini
"Kazi ni msingi wa utu,na kazi ni ibada ukiifanya vizuri unafanya ibada yako vizuri na utapata malipo yako mbele za Mwenyezi Mungu, hatuna budi kuwajibika katika nafasi tulizoaminiwa nazo kwa kufanya kazi kwa uadilifu na kutenda haki kwa wananchi"
Aidha Mhe Mtanda amesisitiza juu ya kuimarisha suala la ushirikiano,mahusiano na mawasiliano kwa watumishi wote kuanzia ngazi ya juu hadi ya chini ili kuweza kuleta tija katika utendaji kazi.
"Tunategemeana hivyo kila mtu apewe thamani yake kulingana na kazi yake kwani inaongeza thamani katika taasisi", amesema Mhe Mtanda.
Aidha Mhe.Mtanda amewataka watumishi wa idara ya ardhi kuwahudumia wananchi kwa haki na kwa wakati huku akisisitiza haki ya kupokelewa,kusikilizwa na kuhudumiwa kwa wateja wote.
Akitoa taarifa ya Manispaa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Bi.Ummy Wayayu amesema kuwa Manispaa yake inao upungufu wa watumishi 1399 katika kada za afya,utawala,kilimo mifugo na uvuvi,elimu,miundombinu,viwanda na biashara pamoja na mipango na uratibu
Akihitimisha kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassan Masala amemshukuru Mhe.Mtanda kwa kutenga muda kuzungumza na watumishi hao na kupokea maelekezo yote aliyoyatoa katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.