“Hakuna mahusiano ya uchaguzi na wafanyabiashara kufanya biashara barabarani, watu wafuate sheria kwani nchi ikienda bila sheria inakuwa ina fujo na nchi yenye fujo haiwezi kuwa nchi endelevu”.
Ni kauli iliyotolewa na Mhe Said Mtanda Mkuu wa Mkoa wa Mwanza tarehe 05 Juni, 2024 alipofika katika soko la Kiloleli katika kata ya Ibungilo kwa lengo la kukagua na kuongea na wafanyabiashara wa soko hilo ambapo amebaini wafanyabiashara wadogo kususia Soko hilo lenye miundombinu rafiki na kujikita kwenye magulio ya mnada yanayofanyika kwenye hifadhi za barabara.
Mhe. Mtanda, amewataka wafanyabiashara wilayani Ilemela kufuata sheria za nchi kwa kufanya shughuli zao kwenye masoko rasmi na kuutaka uongozi wa Wilaya ya Ilemela kusimamia suala hilo kwa kupunguza minada ya barabarani na kuhamasisha wafanyabiashara kubaki kwenye masoko rasmi.
“Mkuu wa Wilaya ninaamini kwamba mtakaa na idara ya biashara kuhakikisha kwamba mnajipanga vizuri kupunguza hiyo minada ili maeneo rasmi yaendelee kuwa na wafanyabiashara”,Amesisitiza Mhe Mtanda
Aidha ametumia mkutano huo kuwakumbusha wafanyabiashara kuwa kufanya biashara katika maeneo rasmi ni fursa kwao, kwani benki ikikukuta eneo rasmi ni rahisi kukukopesha kuliko unapokuwa unafanya biashara kwa kuhamahama hivyo utakuwa hukopesheki.
Sambamba na hilo Mkuu wa Mkoa ametoa mwezi mmoja kwa uongozi wa Ilemela kuhakikisha unatekeleza maelekezo ya kuboresha miundombinu katika soko la kiloleli ili kuweza kuwavutia wafanyabiashara kuuzia bidhaa zao katika soko hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Hassan Masala amesema kuwa wapo tayari kutekeleza maagizo hayo na kwamba wamejipanga kuboresha miundombinu kwenye masoko yao na kwa mwaka wa fedha unaoendelea wametumia zaidi ya Milioni 180 kukarabati miundombinu kwenye masoko lakini bado machinga wamejikita kufanya biashara kwenye hifadhi za barabara kwa kigezo cha mnada.
Kalala Magafu, ni mwenyekiti wa Soko la Kiloleli na mwenyekiti wa wenyeviti wa masoko wilayani Ilemela kwa niaba ya wafanyabiashara wasoko hilo ameomba kufanyike maboresho kama vile kuwekewa umeme, kuongezewa vyoo pamoja na kuwekewa paa eneo la kuuzia ndizi ili kuweza kuwavutia wafanyabiashara wengine kufanyia biashara katika soko hilo, huku akitoa wito kwa wafanyabiashara wenzake kurudi kwenye soko hilo ili maeneo ya nafaka, ndizi, matunda na nguo yapate wafanyabiashara.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.