Watumishi wametakiwa kuwa na nidhamu katika kufanya kazi pamoja na kuhakikisha wanatoa huduma bora ili kuepusha chuki kati ya wananchi na Serikali yao itakayosabababishwa na utendaji kazi mbovu
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhe CPA Amos Gabriel Makalla alipofika kujitambulisha kufuatia kuhamishiwa kwake na Mhe. Rais Mkoani Mwanza mapema mwezi huu.
"Mkiwahudumia vyema mwananchi wataipenda Serikali na kinyume chake wataichukia hivyo tuepushe migogoro na migongano kwenye maeneo yenu ya kutolea huduma.Ipende kazi yako, timiza wajibu wako" CPA Makalla.
Sambamba na hilo CPA Makalla amewataka viongozi wa wilaya ya Ilemela kusimamia masuala ya Usalama wa jamii ili wananchi wawe huru kufanya kazi za kujitafutia maendeleo na kusisitiza kuwa suala la usalama ni kipaumbele chake
"Watu wakikosa usalama watakosa amani ya kufanya mambo ya Maendeleo hivyo lazima tukumbushane umuhimu wa kuwa na amani kwenye maeneo yetu ili kuleta tumaini kwa wananchi kuwa wapo huru kujitafutia kipato." Amesema Makalla.
Vilevile, ameiagiza Halmashauri hiyo kusimamia kwa dhati ukusanyaji wa mapato ya ndani ili wawe na rasilimali za kutosha kutekeleza miradi mbalimbali kwa jamii na kwamba wote kwa pamoja ni lazima wadhibiti Mapato ya ndani na wajiwekee utaratibu wa kujibu Hoja za Ukaguzi kwa wakati.
"Hakikisheni fedha zote zinazokusanywa zinakwenda Benki ili tuweze kujihakikishia ukusanyaji mzuri na kuwahudumia wananchi kwa kutekeleza miradi mbalimbali na wabadhirifu wa fedha wajue kabisa kuwa tunawafuatilia" Amesisitiza.
Nae Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Masala akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya Wilaya ya Ilemela kwa Mkuu wa Mkoa, alisema kuwa wilaya ya Ilemela inaendelea kuboresha mazingira kwa kuwaletea huduma bora za Miundombinu, Elimu na Afya na kwamba makundi yote yanawezeshwa vema kupitia idara ya Maendeleo ya Jamii.
Huku akibainisha kuwa kwa Mwaka wa fedha unaoendelelea (2022/23) Manispaa ya Ilemela ilikadiria kukusanya Shilingi Bilioni 13 na hadi sasa wamekusanya zaidi ya bilioni 14 ambayo ni sawa na asilimia 109 na wanaendelea kutekeleza Miradi yenye thamani ya Bilioni 18.
Akitoa neno la Shukran Naibu Meya wa Manispaa ya Ilemela Mhe Manusura Sadiki amemuomba kusaidia upatikanaji wa mabasi yatakayoanzia safari zake katika kituo kikuu cha malori na mabasi Nyamhongolo ili kuongeza thamani ya fedha zaidi ya bilioni 24.6 zilizotolewa na Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hasan kujenga kituo hicho pamoja na kumhakikishia ushirikiano wa viongozi wa wilaya hiyo katika kuwatumikia wananchi
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.