Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe CPA Amos Makalla ameipongeza Manispaa ya Ilemela kwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya elimu msingi kupitia mradi wa BOOST na kusema kuwa ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo.
Mhe.CPA Amos Makala ametoa pongezi hizo wakati wa hafla ya makabidhiano ya ukamilishaji wa miradi wa BOOST iliyofanyika tarehe 13 Septemba 2023, ambayo ilienda sambamba na .uzinduzi wa Shule mpya ya Msingi ya Buteja ambayo nayo imejengwa kwa fedha za BOOST
Akiongea na wananchi waliofika kushuhudia makabidhiano hayo, amesema kuwa katika Mkoa wa Mwanza Ilemela imekuwa ya kwanza kukabidhi mradi huu wa BOOST na kusema ina maanisha Ilemela inazungumza lugha moja, ameongeza kusema kuwa amekagua madarasa na ameridhishwa nayo.
“Ilemela mmekuwa wa kwanza kukamilisha na kukabidhi mradi huu wa BOOST kwa Mkoa wa Mwanza,maana yake hapa chama na serikali lugha yenu ni moja.Niwashukuru kwa kazi nzuri mliyofanya, nimeenda kwenye madarasa nimeona madawati mazuri nimeona hadi meza na kiti ch mwalimu nimepita sehemu nyingi sijawahi kuona na nimeliona Ilemela kwa mara ya kwanza”, alisema Mhe Makalla
Sambamaba na hilo CPA Makalla amesema kuwa Serikali imetoa fedha nyingi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu mkoani Mwanza, hivyo amewataka wazazi, walezi, walimu na wanafunzi kuhakikisha kuwa utoro haukubaliki Mwanza na kuwa watoto wote wanapaswa kwenda shule.
“Madarasa haya hayatakuwa na maana kama mtoto haendi shule hivyo tuudhibiti utoro sisi wote wanafunzi, wazazi, walimu na walezi wote ni wadau wa kushughulika na suala la utoro”, Alisema CPA Makalla.
Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mhe Hassan Masala Mkuu wa Wilaya ya Ilemela pamoja na kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa fedha alizotoa kutekeleza mradi huu amesema kuwa Wilaya ya Ilemela itaanza kuyatumia madarasa hayo mara tu shule zitakapofunguliwa mwezi huu wa tisa 2023.
“Tumekubaliana sisi kama wilaya madarasa haya 54 yaanze kutumika wiki ijayo punde shule zitakapofunguliwa.” Alisema Mhe. Masala
Nae diwani wa kata ya Kahama Mhe.Samwel Buchenja amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusema kuwa ujio wa shule hii utawezesha mitaa kama mitatu Lukobe,Buteja na Kadinda na kata ya jirani ya Buswelu kunufaika na ukaribu wa shule hiyo kwa kuondoa adha ya watoto kutembea umbali mrefua kufuata shule.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa BOOST, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Adv. Kibamba Kiomoni amesema kuwa lengo kuu la mradi huu wa BOOST ni kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia na kufanikisha upatikanaji wa elimu bora ya awali na msingi sambamba na kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuwezesha wanafunzi kukaa kwa uwiano sahihi wa idadi ya wanafunzi katika vyumba vya madarasa.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ilipokea kiasi cha shilingi 1.57 fedha kutoka Serikali Kuu kupitia mradi wa BOOST ambazo zimetumika kujenga vyumba 54 vya madarasa, vyoo matundu 70, majengo 2 ya utawala, ofisi moja ya mwalimu, madawati 1075, viti na meza 90 vya Elimu ya Awali, viti 74 na meza 74 za walimu, na miundombinu ya viwanja vya michezo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.