Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imetakiwa kuhakikisha inayapima maeneo yote ya taasisi za umma ikiwemo vituo vya afya shule kwa kuziwekea vigingi sambamba na kuziwekea uzio, ili kuepukana na migogoro ya ardhi na uvamizi wa wananchi katika maeneo hayo , kwani ardhi haiongezeki ila watu wanaongezeka
Maagizo hayo yametolewa na Mhe CPA Amos Makalla, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza alipofika katika shule mpya ya sekondari katika kata ya kiseke kwa ajili ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule mpya hiyo ya kimkakati akiwa katika muendelezo wa ziara ya siku mbili ya kusikiliza kero za wananchi na ukaguzi wa miradi ya maendeleo.
“Ipo haja ya kuhakikisha maeneo yote ya umma yanalindwa na kutunzwa, kwani ardhi haiongezeki ila watu wanaongezeka na watu wa siku hizi hawaogopi kuvamia maeneo ya umma, tuyapime maeneo yetu ikibidi tuyawekee na uzio”. Alisema RC Makalla
Aidha Mhe Makalla mbali na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan kwa kutoa fedha za ujenzi wa shule hiyo ameitaka Manispaa ya Ilemela kuacha kujenga majengo ya mtawanyiko badala yake ijenge kuelekea juu (maghorofa) ili kutumia sehemu ndogo ya ardhi na kuwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi.
“Tunapoletewa fedha tujipange kujenga majengo ya ghorofa mwanza haina maeneo mengi ya tambarare ya kujenga miundombinu ya huduma za jamii”, alisema RC Makalla
Mhe. Ramadhan Mwevi ni Diwani wa Kata ya Kiseke, amemshukuru Mhe Rais kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule ya kimkakati katika kata hiyo huku akibainisha umuhimu wa uwepo wa shule hiyo ambapo amesema ujenzi wa shule hiyo utakapokamilika utasaidia kuondoa adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu.
Sambamba na hilo, Mhe Mwevi amesema kuwa kupitia ujenzi wa shule hii ajira mbalimbali zimepatikana ambapo jumla ya mafundi wakuu 7, mafundi wasaidizi 25 na wastani wa vibarua 40 kwa siku wamepata ajira. Pia Mradi umetoa ajira kwa Mama lishe na watoa huduma wengine ambapo wengi wao ni wakazi wa Kata ya Kiseke.
Akisoma taarifa ya mradi Mwalimu Albert Munale ambae ni meneja mradi amesema kuwa kukamilika kwa mradi huu kutaondoa changamoto ya mrundikano wa wanafunzi katika Kata ya Kiseke pamoja na Kata za jirani za Ilemela, Nyasaka, Kawekamo, Kahama na Buswelu kwa kuwa baadhi ya wanafunzi wa shule ya Angelina Mabula watahamishiwa shule mpya na kuongeza ufanisi.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ni kati ya Halmashauri zilizoidhinishwa fedha za ujenzi wa sekondari mpya kupitia Mradi wa SEQUIP kwa mwaka wa Fedha 2022/2023 ambapo ilipokea fedha kutoka Serikali Kuu kiasi cha shilingi milioni 584.28
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.