“Nitoe rai kwa wazazi na wananchi waendelee kuwafichua watoto wenye mahitaji maalum ili na wao wapate haki yao ya msingi ya elimu, kwani baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwaficha watoto wao nyumbani. Niwahikikishie kuwa kwa sasa shule zetu zina mazingira mazuri na rafiki kwa ajili ya watoto hao kusoma na kujifunza”
Rai hiyo imetolewa na mkuu wa divisheni ya elimu ya awali na msingi Mwalimu Mashelo Bahame, wakati wa mapokezi ya vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa ajili ya shule za msingi za manispaa ya ilemela zenye watoto hawa kutoka serikali kuu kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI siku ya Jumatatu ya tarehe 05 Mei 2025.
Pamoja na rai hiyo Mwalimu Mashelo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameendelea kupambania elimu ya watanzania kwani pamoja na vifaa hivyo takriban shilingi milioni 180 zimeshatolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa bweni la Watoto wenye mahitaji maalum ambalo limekamilika likiwa na uwezo wa kubeba wanafunzi 80
Mwalimu Amiri Biliomo kutoka shule ya msingi ya Lake View ametoa shukran zake kwa serikali kwa kuwafikiria wanafunzi hao wenye mahitaji maalum kwani vifaa hivyo vitaenda kuwasaidia katika masomo yao.
“Kiukweli hili ni jambo jema na sisi kama wadau wa elimu tunaiomba serikali iendelee kutoa vifaa hivi kwa watoto hawa ili kuboresha mazingira yao ya kujifunzia na kufundishia” amesema Mwalimu Amiri.
Mwalimu Regina Manyama wa shule ya msingi Ibeshi yenye elimu maalum, ameshukuru kwa vifaa hivyo ambavyo vinaenda kuwarahisishia kazi ya kufundisha katika shule yao ameongeza kusema hii ni mara ya tatu kupokea vifaa hivyo vya Watoto wenye mahitaji maalum.
“Tunaishukuru serikali kwa kuendelea kututhamini na nitasoma kwa bidii ili nami nije niwasaidie wenzangu wenye uhitaji” Ni kauli ya Fatuma Haji mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi Lake View
Nae Elisha Ezekiel, anaesoma shule ya msingi Ibeshi darasa la saba ameishukuru serikali na kuomba kuendelea kupatiwa vifaa hivi ili waweze kusoma vizuri
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imeendelea kupokea vifaa hivi vya wanafunzi wenye mahitaji maalum kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa lengo la kuwaboreshea mazingira ya kujifunzia na kufundishia na hii ikiwa ni mara ya pili katika mwaka wa fedha 2024/2025. Vifaa vilivyopokelewa ni pamoja na mafuta, miwani, kofia kwa ajili ya wanafunzi wenye ualbino pamoja na vifaa vingine kama fimbo kwa watoto wenye ulemavu wa kuona, vifaa vya kurekodi na vingine vinavyotumika na watoto wenye mahitaji maalum.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.