Jamii imeshauriwa kuwajali watoto wenye mahitaji maalum kwa kushiriki utatuzi wa kero na changamoto zao ili waweze kufikia ndoto zao.
Rai hiyo imetolewa na mwakilishi wa mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela ambae pia ni afisa elimu msingi wa manispaa hiyo Mwalimu Mashelo Bahame wakati akipokea msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo Sabuni, Mchele, Mafuta ya kupakaa, Miswaki, Sukari na dawa ya meno kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum wanaosoma shule ya msingi Kirumba kutoka kwa mdau Bi Leah Mihayo.
Aidha Mwalimu Mashelo amempongeza mdau wa maendeleo Bi Leah Mihayo kwa kuguswa na kuwa sehemu ya utatuzi wa kero na changamoto zinazokabili kundi hilo katika jamii huku akiwataka wadau wengine kuiga mfano huo
Amefafanua kuwa Serikali ya Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan imefanya jitihada kubwa kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum wanapata elimu katika mazingira bora na rafiki na kwamba kazi hiyo haiondoi wajibu wa wadau kwa kundi hilo katika jamii.
Akikabidhi msaada huo kwa watoto hao Bi Leah Mihayo amesema kuwa kila mwaka amekuwa na utaratibu wa kutoa sadaka kama sehemu ya kusaidia watoto wenye mahitaji maalum ambapo amekuwa akitoa vitu mbalimbali kwa kadri ya uwezo wake huku akiipongeza manispaa ya Ilemela kwa ushirikiano inaompatia pindi anapoendesha mazoezi hayo huku akiitaka jamii kuyapa kipaumbele makundi yenye mahitaji katika jamii kwa kadri ya nafasi zao.
Sarah Ulimboka ni afisa elimu maalum manispaa ya Ilemela ambapo amesema kuwa mdau wa maendeleo Bi Leah Mihayo ni kiungo muhimu katika kutatua kero na changamoto zinazokabili watoto wenye mahitaji maalum katika wilaya hiyo huku akimshukuru kwa kazi kubwa na nzuri anazozifanya pamoja na kuitaka shule ya msingi Kirumba kushirikiana katika kutatua changamoto za kundi hilo muhimu katika jamii
Nae Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kirumba Michael Menard Mwilenga licha ya kumshukuru mdau huyo kwa msaada wake ameipongeza serikali kwa uwekezaji mkubwa inaoufanya katika kutatua changamoto za watoto wenye mahitaji maalum huku akiomba na watu wengine wenye uwezo kujitokeza kusaidia watoto hao ili kupunguza kero zinazowakabili
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.