Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela, Ndugu Said Kitinga amewataka maafisa ugani kuhakikisha kuwa pikipiki walizopatiwa zinaenda kuleta matokeo chanya katika sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuzitumia kwa malengo mahususi ambayo ni kukuza kilimo kwa asilimia 10 kufikia mwaka 2030.
Akikabidhi pikipiki hizo kwa maafisa ugani kilimo 38 Ndugu Kitinga amewataka kuwafikia wakulima sehemu zote, jambo ambalo llitawasaidia na kuwainua vijana waliojiajiri katika kilimo kwa kuwapatia maarifa juu ya masuala mbalimbali ya kilimo ikiwa ni pamoja kufanya kazi kwa ueledi.
“Pikipiki hizi ni nyenzo muhimu katika moja ya vifaa mnavyovihitaji na zitawasaidia katika kuwafikia wananchi popote walipo ili kuwafundisha kilimo cha kibiashara na mwisho wa siku waweze kufanya kazi kwa tija”, amesema Ndugu Kitinga
Mhe Rais wakati anakabidhi vifaa hivi pale Dodoma aliwataka mtakapokabidhiwa pikipiki hizi muende mkazitunze na kuzitunza si kuziweka ndani bali ni kuzifanyia matengenezo kwa wakati huku akiwataka kmkazitumie kwa malengo mahususi ambayo yamekusudiwa ya kuwafikia wananchi katika maeneo yenu ya kazi” alinukuu Ndugu Kitinga
Aliongeza kusema kuwa ni matumaini yake kuwa kupatikana kwa pikipiki hizi kutasaidia kuwainua vijana ambao wamejiajiri katika suala la kilimo ili waweze kupata maarifa na kuweza kuwavutia vijana wengi kuingia katika shughuli za kilimo na mwisho wa siku watafanya shughuli zao kitaalamu zaidi na watainua uchumi wao pamoja na kujiajiri.
Akimkaribisha Katibu Tawala, mkurugenzi wa Manispaa Mhandisi Modest Apolinary, amewataka maafisa ugani hao kuhakikisha pikipiki hizo zinaenda kuwasaidia wakulima katika maeneo yote ambao yalikuwa hayafikiki kwa wakati na kuwataka kuanza kazi mara moja.
Neema Semwaiko ni Mkuu wa Divisheni ya kilimo ,mifugo na uvuvi na pia ni afisa kilimo Manispaa ya Ilemela pamoja na kumshukuru Mhe Rais kwa kuwafikia amemshukuru pia waziri wa kilimo ambae amesaidia upatikanaji wa pikipiki hizi na kusema kuwa ni jambo la kihistoria.
“Binafsi nimefanya kazi zaidi ya miaka 30 lakini tulikuwa hatujawahi kupata pikipiki kwa mkupuo kama tulivyopata hivyo tunamuahidi Mhe Rais kwamba hizi pikipiki tunaenda kuzitumia kwa malengo husika, tutaongeza uzalishaji na tutazitumia kwa ukamilifu kwa kuwafikia wakulima wengi zaidi ili kuweza kuongeza uzalishaji ili kufikia lengo la serikali kwamba kufikia 2030 kilimo kiwe kimekua kwa asilimia kumi”, amesema Bi Semwaiko
Nae Tumaini Lushinde afia kilimo kata ya Sangabuye kwa niaba ya wenzake ameahidi kuvitunza vifaa hivi na kusema kuwa vitaleta tija upande wa kilimo hususan kwa kuwatembelea wakulima na kuwapa mbinu za kilimo bora akiahidi kutoka hapo walipo na kufika katika kiwango kilichokusudiwa kwa ajili ya kuweza kuwainua wakulima.
Jumla ya pikipiki 38 zimekabidhiwa kwa maafisa ugani kilimo 38, kutoka serikali kuu kupitia wizara ya kilimo kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali za sekta ya kilimo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.