Jamii ya Ilemela imeaswa kuzingatia lishe bora kwa makundi yote ya watu kuanzia ngazi ya familia.
Hayo yamesemwa na Joyce Albert Afisa lishe wa kituo cha Afya Buzuruga wakati akiongea wananchi wa kata ya Sangabuye katika mtaa wa Igalagala katika maadhimisho ya siku ya afya ya lishe kwa mtaa (SALIM).
Bi.Joyce amewataka watu wote ndani ya jamii wenye uelewa timamu kufuatilia masuala ya lishe kwa familia nzima.
"... Watoto,kina mama wajawazito, wazee wote ni makundi yanayohitaji kupata lishe kwa kuzingatia makundi matano ya vyakula kwa kipimo sahihi,tusimuachie mama peke yake hata kina baba mna nafasi yenu katika kuhakikisha familia inapata huduma zote za kiafya ikiwemo lishe bora."
Maadhimisho hayo ya SALIM yamekuwa ya kipekee kwa kusindikizwa na kipengele cha jiko darasa ambapo wananchi wamepata fursa ya kufundishwa kwa vitendo namna bora ya kupika lishe kamili kwa uwiano sahihi wa makundi yote ya vyakula.
Nae Mhudumu kiongozi wa huduma za afya mtaa wa Igalagala Moses Madashi amesema maadhimisho hayo yameongeza chachu ya jamii yao kuhudhuria kwenye vituo vya kutolea huduma na kupata huduma mbalimbali za afya jambo linalozidi kuimarisha afya zao.
Akihitimisha maadhimisho hayo mwenyekiti wa mtaa wa Igalagala Yulita Simon amewataka wananchi wake kuzingatia mlo kamili, watoto kupata chanjo,kina mama wajawazito kuanza kujifuatilia mapema kwa kuhudhuria kliniki punde wanapojigundua ni wajawazito na kunywa maji safi na salama ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuwa na jamii salama yenye afya nzuri.
" Elimu na huduma za afya tulizozipata ni msaada mkubwa sana kwetu, nilikuwa nakula kushiba bila kujali vipimo sahihi vya makundi ya vyakula." Amesema Veronica Budodi mkazi wa Igalagala
|
|
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.