Naibu Waziri OR-TAMISEMI, Mhe. Josephat Kandege (Mb), ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa muitikio wa wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuzitaka halmashauri zingine kuja kujifunza namna ambavyo halmashauri imeweza kuwaleta wananchi pamoja na kuweza kushirikiana nao katika suala zima la maendeleo.
“Nitoe wito kwa halmashauri zingine kuja kujifunza namna ushirikiano huu umewezakana kwani mwitiko wa wananchi umekuwa mkubwa sana katika kutekeleza miradi ya maendeleo hususani ujenzi wa vyumba vya madarasa pamoja na miradi mingine inayojitokeza. Niwasihi wananchi kuendelea kujitoa katika suala zima la maendeleo kwani maendeleo ni ya kwetu sote”, Alisisitiza
Mhe. Kandege aliyasema hayo alipokuwa katika ziara ya kikazi kwa ajili ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ambapo pia alipata fursa ya kuzungumza na watumishi wa manispaa.
Akiongea na watumishi aligusia suala la elimu ambapo aliipongeza Halmashauri kwa kushika nafasi ya pili kitaifa katika matokeo ya darasa la saba kwa mwaka 2019. Huku akiwaelekeza Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi kuhakikisha kuwa watoto wote waliofaulu wanaingia kidato cha kwanza na iwapo watakuwepo watoto ambao hawajaripoti basi wazazi wa watoto hao wakamatwe.
Pia alitoa pongezi kwa Halmashauri kwa kupata hati safi mara tano mfululizo na kusema kuwa halmashauri yoyote inayopata hati safi ni wazi kuwa mkaguzi wa ndani anatekeleza majukumu yake ipasavyo na pia Mkurugenzi anakuwa anajitambua kwani anakuwa anafuata ushauri wa mkaguzi wa ndani .
Mhe Kandege aliendelea kusema kuwa ameridhishwa na utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo kwani hakuna mradi ambao ametembelea hajaridhika nao huku akielekeza masuala mbalimbali hususani suala la utoaji mikopo ambapo alielekeza kuwa, halmashauri ihakikishe kuwa inatenga pesa ya kutosha na kutoa pesa ya kiwango kikubwa ili kuviwezesha vikundi hivyo kutekeleza miradi mikubwa yenye kuleta tija na kuweza kuondoa hali duni ya maisha kwa wananchi wa Ilemela.
Ameyasema hayo alipotembelea kikundi cha wanawake ambacho kinapata mkopo kutoka Ilemela ambapo alishauri kuwa pindi watakapomaliza mkopo walionao Mkurugenzi ahakikishe anawapa mkopo wa Mil 20 ili kuwawezesha kufanya ujasiriamali wa kiwango kikubwa.
Sambamba na hilo alitoa maelekezo akiwa katika shule ya sekondari ya Buswelu na kumuelekeza mkurugenzi kuhakikisha kuwa anakamilisha kazi zilizobakia ili kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri.
Nae Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Ndugu John Wanga alimshukuru Naibu Waziri kwa kutembelea halmashauri yake na kuahidi kutekeleza maelekezo yote aliyoyatoa kwani jukumu kubwa ni kuhakikisha kuwa miradi inatekelezwa ili kuweza kuwaondolea wananchi adha mbalimbali, huku akimshukuru Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipatia pesa Manispaa ya Ilemela kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa kimkakati wa stendi ya mabasi na eneo la uegeshaji wa malori kwani mradi utakapokamilika utaongeza mapato kwa Halmashauri.
Akiwa katika Manispaa ya Ilemela Mhe. Josephat Kandege alikagua miradi ya ufyatuaji wa matofali unaomilikiwa na halmashauri, shule ya Sekondari Buswelu, mradi wa barabara ya Sabasaba-Kiseke-Buswelu na barabara ya Makongoro junction-Mwaloni. Pia alipata fursa ya kukagua kikundi cha wanawake wanaopata mkopo toka halmashauri, pamoja na mradi wa kimkakati wa ujenzi wa stendi ya mabasi na maegesho ya malori uliopo Nyamhongolo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.