Ndugu Mary Chatanda, ambae ni Mwenyekiti wa UWT Taifa ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa wilayani Ilemela. Amebainisha hayo akiwa katika ziara ya kikazi wilayani humu yenye lengo la kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM sambamba na kulinganisha thamani ya fedha iliyotumika katika miradi hiyo.
Akiwa wilayani Ilemela amekagua bweni la wasichana katika shule ya sekondari ya Bwiru lililojengwa kwa fedha za mradi wa SEQUIP kiasi cha Shilingi milioni 130 pamoja na Shule mpya ya Sekondari ya Kisenga iliyopo kata ya Kiseke iliyojengwa kwa fedha za EP4R kiasi cha Shilingi Milioni ambapo amepongeza jitihada za serikali na kuelekeza miundombinu hiyo ya shule kutunzwa.
Sambamba na ukaguzi wa miradi ya elimu alikagua ujenzi wa barabara ya Buswelu Nyamadoke Nyamhongolo (km 9.5) inayojengwa kwa fedha kutoka benki ya dunia, ambapo Ndugu Chatanda amemtaka mkandarasi kuhakikisha anaijenga barabara hiyo kwa viwango na kuikamilisha kwa wakati uliopangwa ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
Ndugu Chatanda katika nyakati tofauti alipata wasaa wa kuwahutubia wanachi wa kata za Pasiansi, Kitangiri na Kawekamo ambapo alisisitiza juu ya suala la kuporomoka kwa maadili na kuwataka wazazi kuhakikisha wanawasimamia wao na kushirikiana na walimu katika malezi hayo huku akiwataka watoto wa kiume na wa kike kuhakikisha wanazingatia masomo na kuachana na mambo ya kidunia.
Kuhusu mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri amemuelekeza Mkurugenzi kuhakikisha maafisa maendeleo ya jamii kutoa mafunzo ya matumizi bora ya mikopo kabla ya kutoa mikopo kwa walengwa ili mikopo hiyo ilete tija kwao.
Sambamba na hayo Ndugu Chatanda amewataka wana Ilemela kuhakikisha wanashiriki zoezi la uboreshaji wa taarifa katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu 2025.
Nae mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amemuomba ndugu Chatanda kufikisha salam za shukrani kwa Rais Samia kwa fedha nyingi alizotoa jimboni humo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi akizitaja kuwa ni takribani shilingi bilioni 69 zimepokelewa katika kipindi cha miaka mitatu.
Ziara hiyo imejumuisha wajumbe wa kamati ya utekelezaji ya Baraza kuu Taifa na viongozi mbalimbali wa UWT ambapo nao walipata wasaa wakukagua miradi katika kata mbalimbali ndani ya wilaya ya Ilemela ikihusisha miradi ya sekta za Afya, elimu na miundombinu ya Barabara.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.