Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 ukiongozwa na Ndugu Abdalla Shaib Kaim umeridhishwa na utekelezaji wa miradi yote ambayo imepitiwa na Mwenge wa Uhuru yenye thamani ya fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 1.35
Akiongea na hadhara ya wananchi wa Wilaya ya Ilemela katika viwanja vya furahisha, Ndugu Abdalla ameipongeza Ilemela kwa kuwa na miradi mizuri ambayo imezingatia viwango pamoja na thamani ya fedha, huku akisisitiza kuhakikisha kuwa maelekezo yote yaliyotolewa yanafanyiwa kazi.
Awali akizindua barabara za mitaa ya Kirumba (Magomeni,Kabuhoro hadi ziwani zenye urefu wa Km. 0.9 amepongeza kwa mradi mzuri na kuhimiza kuwa barabara itunzwe ili iweze kuwa imara na madhubuti ili iweze kutumika kwa muda mrefu na kwa maslahi mapana ya wana Ilemela na watanzania kwa ujumla
Akiwa katika Shule wa sekondari ya wavulana Bwiru Ndugu Abdalla ameridhishwa na kuipongeza Ilemela kwa namna ambavyo imeweza kuendana na Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 isemayo, “ Tunza Mazingira, Okoa Vyanzo vya Maji kwa ustawi wa Viumbe hai kwa Uchumi wa Taifa” kwa kupanda miti mingi ikiashiria kuwa Ilemela inaunga jitihada za serikali za kukabiliana na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi ambapo amewaongoza wakimbiza Mwenge kitaifa pamoja na viongozi mbalimbali kupanda miti 500.
Mwenge wa Uhuru ukikimbizwa Wilayani Ilemela umepitia mradi wa udhibiti taka ngumu ambapo Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Ndugu Abdalla Shaib Kaim, amekabidhi vifaa vya usafi kwa viongozi wa soko la Kiloleli na amewahimiza kuendelea kuunga mkono juhudi zinazoendelea za utunzaji wa mazingira kwa kuhamasisha utunzaji na usafi wa mazingira kuepukana na utupaji wa taka hovyo na matumizi ya plastic.
Akikagua mradi wa vijana wa ufugaji kuku ambao umepatiwa mkopo kiasi cha Shilingi Milioni 15 unaotokana na mapato ya ndani ya Manispaa ya Ilemela, kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru ameipongeza Ilemela kwa kutenga fedha zinazotokana na mapato ya ndani kwa ajili ya kukopesha makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu huku akitoa wito kwa vikundi vyote vinavyonufaika na fedha za mikopo kufanya marejesho ili vikundi vingine viweze kunufaika.
Sambamba na hilo Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 Ndugu Abdalla amezindua jengo la mama na mtoto katika kituo cha afya Buzuruga lililojengwa na fedha za mapato ya ndani kiasi cha shilingi Milioni 199 pamoja na kugawa vyandarua kwa makundi mbalimbali ikiwa ni jitihada za serikali za kutokomeza ugonjwa wa malaria chini ya kauli mbiu isemayo “Ziro Malaria inaanza na mimi;nachukua hatua kuitokomeza”
Halikadhalika Ndugu Abdalla ameutaka uongozi wa Ilemela kuhakikisha ujenzi wa bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum unakamilika kwa wakati na kwa viwango kwa kuzingatia thamani ya fedha ili kuhakikisha dhamira ya serikali ya kuhudumia kundi hili muhimu linatimia, ameyasema haya wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika ujenzi wa bweni hilo ambalo hadi kukamilika kwake litagharimu kiasi cha shilingi milioni 100 fedha kutoka serikali kuu.
Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Mhe Angeline Mabula amemshukuru Rais, Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi kupitia sekta mbalimbali kwani fedha hizo zimetumika katika utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakumba wananchi wa Ilemela
Mwenge wa Uhuru 2023 umekimbizwa umbali wa Kilometa 57 ukieneza kauli mbiu ya : " Tunza Mazingira, Okoa Vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe Hai kwa Uchumi wa Taifa." ambapo umezindua miradi miwili, umeweka jiwe la msingi kwenye mradi mmoja na umekagua mradi mmoja.Pamoja na miradi hiyo Mwenge umekagua shughuli saba.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.