Halmashauri ya wilaya ya Mufindi imevutiwa na kupongeza miradi ya sekta ya uvuvi ya ufugaji samaki kwa njia ya vizimba inayotekelezwa kata ya Sangabuye eneo la Igalagala na biashara ya mazao ya samaki katika soko la kimataifa la Kirumba ndani ya manispaa ya Ilemela.
Akizungumza wakati wa ziara ya madiwani wa manispaa ya Mufindi kwa ajili ya kujifunza namna sekta ya uvuvi inavyoweza kuongeza mapato ya halmashauri Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Mhe. Festo Elia Mgina amesema kuwa amefurahisha na namna manispaa ya Ilemela inavyonufaika na mapato ya sekta ya uvuvi kutokana na uwekezaji iliyoufanya huku akiwaasa madiwani wenzake kuona namna bora ya wao kuweka mipango na mikakati katika mwaka wa fedha ujao kuwekeza katika ufugaji samaki wa mabwawa ili nao waweze kuongeza mapato ya Halmashauri yao na uchumi wa mwananchi mmoja mmoja .
"..Tumefarijika sana kwa maelekezo yenu pamoja na namna mradi wa vizimba vya ufugaji samaki unavyotekelezwa, Kwa niaba ya wenzangu tunawashukuru sana.." Alisema
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi Mhe. Boniphace Castory Masangula mbali na kuipongeza manispaa ya Ilemela ameongeza kuwa wilaya ya Mufindi ina mabwawa ya Ngwaki, Kihanga na Nzili hivyo kama watazingatia walichojifunza, elimu waliyoipata itasaidia katika kutekeleza miradi ya uvuvi na mazao ya samaki kwa ufanisi zaidi.
Nae Mkurugenzi wa Wilaya ya Mufindi Ndugu Mashaka Said Mfaume akaongeza kuwa ziara waliyoifanya imewasaidia kuongeza maarifa mapya ambayo hawakuwa nayo ikiwemo ufugaji wa samaki Kwa njia ya vizimba unavuofanyika, ulishaji wa samaki, uvunaji wa samaki na makadirio ya chakula cha samaki elimu ambayo itawasaidia watakapoanza kutekeleza miradi ya uvuvi.
Mhe Renatus Bahebe Mulunga ni Mstahiki meya wa manispaa ya Ilemela ambapo amesema kuwa mafanikio yanayopatikana ndani ya manispaa yake ni matokeo ya kauli mbiu ya wilaya hiyo ya 'Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga' ambapo suala la maendeleo linalopangwa na mbunge ndilo la meya, ndilo la mkurugenzi, ndilo la chama tawala, ndilo la mkuu wa wilaya, ndilo la madiwani hivyo kurahisisha juhudi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo huku akiwaasa watu wa Mufindi kuwa na kauli mbiu inayowaunganisha wananchi na viongozi katika kuchochea maendeleo .
|
|
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.