Waheshimiwa Madiwani wa Manispaa ya Ilemela wametakiwa kuhakikisha wanakuwa makini na kuwa mstari wa mbele katika kuunga juhudi zinazoendelea za kuweka mji safi katika manispaa ya Ilemela.
Rai hiyo imetolewa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela Mhe Renatus Mulunga wakati wa kikao cha baraza la madiwani cha kupokea taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa kata 19.
Aidha Mhe Mulunga amezitaka kampuni zinazotekeleza shughuli za usafi na mazingira ndani ya Manispaa ya Ilemela kuhakikisha zinatekeleza wajibu wake ikiwa ni pamoja na kuwasilisha fedha za tozo za usafi za asilimia thelathini ya jumla ya kiasi chote kinachokusanywa kama inavyoelekeza sheria ndogo za ada na ushuru za Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela za mwaka 2022 .
Pamoja na hayo amewaelekeza waheshimiwa madiwani kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa makampuni ya usafi yanawasilisha asilimia thelathini ya fedha yote inayokusanywa kupitia uzoaji taka kama sheria inavyoelekeza na kwamba manispaa haitazifumbia macho kampuni zitakazoshindwa kufanya hivyo
“Kawaambieni wenye makampuni ya usafi katika maeneo yenu kuwa wanawajibu wa kuwasilisha ile asilimia thelathini, Na nyinyi niwaombe mkawasimamie hatutakuwa na mzaha katika hili”, Alisema
Kuhusu ujenzi wa vyumba 110 vya madarasa unaoendelea kupitia fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 2.2 zilizotolewa na Rais Samia, Mhe Mulunga amewahimiza waheshimiwa madiwani kushiriki kikamilifu katika shughuli za ujenzi huo ili kuunga juhudi za Mhe Rais kwa kuhakikisha kuwa fedha hiyo inatendewa haki.
Kupitia baraza hilo la Kata waheshimiwa madiwani kwa nyakati tofauti wametumia nafasi hiyo kumshukuru Mhe Samia Suluhu Hassan , Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 110 vya madarasa katika shule 23 za sekondari katika kata 19 za Ilemela.
Nae mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary amewasihi madiwani na wataalam wa kata kuhakikisha wanaweka kwenye mpango wa bajeti vipaumbele vyao vya utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa ajili ya maandalizi ya bajeti yam waka wa fedha ujao kwani vipaumbele vyote huibuliwa kutoka kwenye kata zao.
Mkutano wa Baraza la kata hufanyika kila robo ya mwaka wa fedha ambapo waheshimiwa madiwani huwasilisha taarifa za utekelezaji katika kata zao ikiwemo na changamoto mbalimbali zinazokabili kata zao kwa kuonyesha ni namna gani wameweza kuzitatua na kwa ambazo zimeshindikana huwasilishwa kwa Mkurugenzi kwa ajili ya kuzipatia ufumbuzi.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.