Mhe. Dkt Severine Mathias Lalika, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela amewataka wananchi wa Ilemela kutokulionea aibu suala la kujiunga na elimu ya watu wazima.
Ameyasema hayo katika maadhimisho ya juma la elimu ambalo huadhimishwa kuanzia tarehe 01 hadi tarehe 08 mwezi wa tisa ya kila mwaka.
“Wananchi msione aibu kujifunza, Halmashauri yetu inao mfumo mzuri wa utoaji wa elimu kwa watu wazima. Na ni jukumu letu sote kuhamasisha wahitaji wa elimu ya watu wazima kujiunga na mipango mbalimbali inayoendelea kufanya kazi ndani ya Halmashauri ikiwa ni pamoja na Mpango wa uwiano kati ya elimu ya watu wazima na jamii (MUKEJA),Mpango wa elimu ya Msingi kwa walioikosa (MEMKWA),Elimu Masafa na Masomo ya ana kwa ana -Open and Distance Learning(ODL) na elimu ya ufundi.Tusiogope tuchangamkie fursa zilizopo kwa manufaa ya jamii yetu” alisema .
Aidha alisema kuwa wilaya yake inatambua uwepo wa watu wazima wasiojua kusoma na kuandika na kumtaka Mkurugenzi wa Manispaa kuendelea na mikakati ya kuhakikisha watu wake wote wanajua kusoma na kuandika kupitia njia mbalimbali za kutoa elimu kwa njia rahisi ili watu wazima waweze kuelewa na kujifunza haraka.
“Katika nyakati hizi nchi zote duniani ikiwemo Tanzania, zinafanya bidii kuhakikisha watu wake wote wanapata elimu iliyo bora bila kujali jinsia kwa kuwa elimu ni moja ya haki za msingi za binadamu. Elimu inawasaidia wanadamu kuendana na mabadiliko yanayotokea hapa duniani”.Alisisitiza
Nae Mkuu wa idara ya elimu msingi katika Manispaa ya Ilemela Ndugu Isack Busungu amesema kuwa elimu haina mwisho na ni muhimu watu wote kupata elimu ya utambuzi wa vitu mbalimbali katika maisha ya kawaida ya mwanadamu.
Pamoja na hayo alisema kuwa Manispaa ya Ilemela inaendelea kusimamia masuala mbalimbali ya mpango wa elimu kwa walioikosa (MEMKWA), mpaka sasa manispaa ina jumla ya wanafunzi 977 ambapo wavulana ni 535 na wasichana 442, kati yao jumla ya wanafunzi 79 wamehitimu elimu ya msingi 2019 na kuingia kadato cha kwanza 2020 ambapo wavulana ni 45 na wasichana ni 34.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imeungana na Halmashauri zingine nchini katika kuadhimisha juma la elimu ya watu wazima linaloadhimishwa kila mwaka tarehe 01 hadi 08 Septemba duniani mwaka huu iliyobebwa na kauli mbiu ‘Elimu ya watu wazima ituwezeshe kuwachagua viongozi bora watakao tuletea maendeleo’.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.