Mradi wa ufyatuaji wa matofali wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ni mradi ulioibuliwa kwa ajili ya kutanua wigo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri na hatimae kupunguza utegemezi wa Halmashauri kutoka Serikali Kuu na halikadhalika kuwezesha upatikanaji wa matofali ya ujenzi wa miundo mbinu katika sekta mbalimbali hususan elimu na afya.
Chimbuko la mradi huu ni mipango ya maendeleo ya halmshauri ya Manispaa ya Ilemela kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kutumia mapato ya ndani. Katika kupunguza gharama na pia kurahisha ujenzi wa miundo mbinu ya umma.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kupitia fedha za makusanyo ya ndani iliamua kununua mashine ya kisasa ambayo iligharimu kiasi cha Fedha za kitanzania shilingi 70,266,000.00.
Lengo kubwa la ununuzi wa mashine lilikuwa ni kuanzisha mradi ya ufyatuaji matofali kwa ajili ya kuzalisha tofali za kukamilisha miundo mbinu ya Elimu na Afya ikiwa ni njia mojawapo ya kuunga mkono jitihada za wananchi kwa kuboresha miundo mbinu ya Elimu na Afya.
Pamoja na hilo pia, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela inatarajia kusajili rasmi mradi huu ili uweze kuwa mradi wa kibiashara ambapo utakuwa chanzo mojawapo cha kuingizia mapato katika halmashauri ili kuweza kupunguza utegemezi wa Manispaa ya Ilemela kwa Serikali Kuu katika bajeti ya Maendeleo.
Shughuli za uzalishaji wa matofali zilianza rasmi tarehe 4/2/2020 ambapo hadi kufikia tarehe 30/6/2020 jumla ya matofali 115,292 yenye thamani ya shilingi 135,066,000 milioni yamezalishwa. Kati ya hayo, matofali 63,837 yenye thamani ya shilingi 72,700,700 milioni yamesambazwa mashuleni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa,ukamilishaji wa Hospitali ya Wilaya, ujenzi wa zahanati ya Nyamadoke,ujenzi wa ofisi ya Kata Bugogwa na matofali 39,955 yameuzwa kwa taasisi jirani .
Mashine hii inayo uwezo wa kufyatua matofali ya inchi sita (6) na inchi tano(5) pamoja na kuzalisha matofali 5000 kwa siku sawa na asilimia 100 ya uwezo wa mashine. Aidha kutokana na upungufu wa vibao vya kufyatulia matofali kwa sasa huzalisha jumla ya matofali 2500, kutatua changamoto hii halmashauri inafanya utaratibu wa kuagiza vibao vingine.
Yapo mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kupitia mradi huu wa ufyatuaji wa matofali ambayo ni pamoja; Mradi umewezesha kuchangia tofali 63,837 katika ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule 17 za sekondari, shule 4 za Msingi, ofisi ya Kata Bugogwa, Zahanati ya Nyamadoke na Hospitali ya Wilaya ya Ilemela.Pia Mradi umetoa ajira kwa vijana 18 na mama lishe 3 ambao wameweza kujiongezea kipato pamoja na kutoa fursa ya kazi kwa wamiliki 6 wa malori wanaosomba matofali na mchanga katika mradi.
Ununuzi wa mashine hii ya kufyatulia matofali yalikuwa maamuzi ya baraza la Waheshimiwa Madiwani (2015/2020) lililomaliza muda wake na wataalamu wa Halmashauri ya Manispaaa ya Ilemela baada ya kufanya ziara ya kimafunzo katika Jiji la Tanga na kujionea hatua za kimaendeleo zilizopatikana kutokana na mradi wa ufyatuaji wa tofali.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.