Daktari Severine Lalika, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela amefunga rasmi mashindano ya UMISETA yaliyofanyka kwa muda wa siku 3 kuanzia tarehe 22hadi tarehe 24 Mwezi wa tano yaliyokuwa yakifanyika katika shule ya sekondari ya wavulana Bwiru.
Mashindano ya UMISETA ni Umoja wa Michezo Shule za Sekondari Tanzania ambayo hukutanisha shule za sekondari mbalimbali nchini. ambapo kwa wilaya ya Ilemela Mashindano hayo yalihusisha timu za kutoka shule za kanda nne za Bugogwa, Buswelu, Bwiru na Pasiansi ambapo jumla ya michezo 8 ilishindaniwa ikiwemo mpira wa Miguu,pete, kikapu, mikono, wavu, meza, riadha na sanaa za maonesho.
Akifunga mashindano hayo, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela amewataka wanafunzi waliochaguliwa kuunda timu ya wilaya kwa ajili ya kwenda kushiriki mashindano ya UMISETA ngazi ya Mkoa kuhakikisha wanarudi na ushindi na kuijengea heshima wilaya yao kwa kuwa na nidhamu na weledi.
Aliendelea kwa kusema kuwa, Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Mhe Dkt John Magufuli itaendelea kuimarisha michezo mashuleni ili kusaidia vijana waweze kujiajiri, kuimarisha afya zao na kuwaepusha kujiingiza katika mambo yasiyo faa ikiwemo vitendo vya uhalifu na matumizi ya madawa ya kulevya.
Nae afisa elimu sekondari Manispaa ya Ilemela Ndugu Emanuel Malima amemuhakikishia Mkuu wa Wilaya ushindi kwa timu hiyo inayokwenda kushiriki ngazi ya mkoa sambamba na kumshukuru mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa ufadhili alioutoa wa ununuzi wa baadhi ya vifaa vya michezo katika mashindano hayo ikiwemo jezi.
Katika mashindano hayo kwa mwaka huu wa 2019 Timu ya Kanda ya Bugogwa iliibuka mshindi wa jumla wa mashindano ikiwa ni miaka miwili mfululizo ikifuatiwa na timu ya kanda ya Pasiansi, Bwiru na wa mwisho Buswelu kisha kukabidhiwa kombe la jumla la ushindi kama zawadi.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.