Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe.Mathias Severine Lalika ametoa tahadhari kwa wananchi wa Ilemela alipotembelea katika eneo la kituo tengefu “Isolation centre”lililopo ndani ya kata ya Kahama iliyopo wilayani Ilemela.
Akizungumza katika eneo tengefu kwa ajili ya wagonjwa wa watakaoathiriwa na virusi vya Corona “COVID-19” Mhe .Lalika ametoa tahadhari kwa wakazi na wageni wanaoingia Wilayani Ilemela juu ya kujikinga na virusi vya Corona kuwa wanatakiwa kudumisha usafi kwa kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi na sabuni na kupenda kutumia vitakasa mikono “sanitizer” ,kufunika mdomo na pua wakati wa kukohoa au kupiga chafya kwa kutumia kitambaa chepesi au kwenye nguo uliyovaa sehemu ya mkono.
Aidha amezitaka taasisi zote za umma ndani ya Wilaya ya Ilemela kuweka maji safi yanayotiririka katika maeneo ya kutolea huduma zao mbalimbali.
Sambamba na hilo Mhe.amewataka wakazi wa Ilemela kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima kama vile misiba,harusi ,vikao vya kijamii,ibada misikitini na makanisani huku akishauri ushiriki wa watu wachache katika matukio ya lazima kama misiba.
“Mabanda wanayoonyesha video,mipira na sinema waache mara moja maana ni maeneo hatarishi kwani yanaruhusu kusambaa kwa kasi maambukizi ya virusi vya corona.”Alisisitiza Mhe.lalika.
Pamoja na hayo Mkuu wa Wilaya, amewataka watumiaji na wamiliki wa usafiri wa umma kupakia abiria sawa sawa na uwezo wa chombo husika “level seat”na abiria waepuke kupanda magari yaliyojaa kupita kiasi.
Aidha alitumia fursa hiyo kuwapongeza na kuwatia moyo wataalam wa afya kwa namna wanavyojitoa kwa ajili ya kuokoa maisha ya wagonjwa watakaobainika kuwa na virusi hivi vya corona kwani ni kazi ngumu ambayo inahitaji kujitoa zaidi, alisema kuwa serikali inatambua hilo na tupo pamoja katika kufanikisha hili.
Mhe.Lalika amehitimisha kwa kuwataka wananchi wote kufuatilia kwa karibu juu ya afya zao na kufuata maelekezo ya wataalam wa afya katika kujilinda na maambukizi ya virusi vya corona. “Kinga ni bora kuliko tiba”
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.