Mhe Adam Malima Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ameipongeza Manispaa ya Ilemela kwa ukamilishaji wa vyumba 110 vya madarasa vikiwa na seti 5500 za meza na viti kwa gharama ya kiasi cha Shilingi bilioni mbili na milioni mia mbili fedha iliyotolewa na serikali kuu.
Mhe. Malima ametoa pongezi hizo wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya vyumba vya madarasa hayo mara baada ya ujenzi kukamilika huku akihimiza suala la ukamilishaji wa vyumba vya madarasa ambavyo vimejengwa kwa nguvu za wananchi wa Ilemela ili kuweza kuwatendea haki wanafunzi ambapo ametumia fursa hiyo kuwashukuru na kuwapongeza wananchi wa Ilemela kwa kujenga madarasa 130.
“Katika wilaya zote za Mkoa wa Mwanza, Ilemela mmewapita wote, kwa hili naomba niwapongeze sana lakini naomba nirejee kama tunakuja kupongezana kwa madarasa haya mapya na hatutengi kwenye bajeti zetu marekebisho ya madarasa ya zamani tutakuwa hatutendi haki kwa wanafunzi wanaosoma katika madarasa hayo kwani bila madarasa yale tusingekuwa na haya madarasa 110, amesema Mhe Malima
Pamoja na hayo ameutaka uongozi wa Ilemela kuanza kufikiria suala la matumizi bora ya ardhi kwa kuanza kujenga majengo ya ghorofa ili kuweza kutunza ardhi na kuhifadhi maeneo ya kuchezea watoto na kusisitiza kuwa Mwanza ni mji wa kisasa hivyo mambo yake lazima yaende kisasa.
“Kauli mbiu yangu mimi ni kwamba Mwanza ni mji wa kisasa hivyo lazima mambo yake yawe ya kisasa mnapowaza mambo ya mwanza wazeni kisasa, huko mbele tunapoenda tuanze kufikiria changamoto zinazokuja kwa kufikiria matumizi ya nafasi katika shule zenu kwa maana kuangalia ujenzi wa ghorofa kwa ajili ya kutunza matumizi ya ardhi”, amesema Mhe Malima
Ndugu Balandya Elikana, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza akimkaribisha Mkuu wa Mkoa amewataka viongozi na wananchi kwa pamoja kushirikiana na kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2023 wanaripoti shule mara ifikapo tarehe 09 Januari 2023.
“Ni jukumu kwetu sisi viongozi na wananchi kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa wanajiunga na kidato cha kwanza tushirikiane na tuwahimize vijana wetu kujiunga na kidato cha kwanza na hakuna kitu cha urithi utakachomuachia mtoto isipokuwa elimu na Mhe Rais Dkt Samiah Hassan anafanya kazi kubwa na anaendelea kutoa kipaumbele katika elimu ni muhimu kumuunga mkono kwa kazi kubwa anayofanya lakini tutakuwa tumemuunga mkono kwa kuhakikisha kuwa wote waliochaguliwa kidato cha kwanza wamejiunga, madarasa haya hayatakuwa na maana kama yatabaki matupu hivyo tushirikiane sote kuhakikisha kuwa wanafunzi wanajiunga”, amesema Ndugu Balandya
Akisoma taarifa ya makabidhiano Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary amebainisha kuwa mahitaji ya madarasa kwa kidato cha kwanza kwa mwaka 2023 ni vyumba vya madarasa 252 kwa ajili ya wanafunzi 12,548 ambapo wasichana ni 6537 na wavulana 6011 , vyumba vilivyokuwepo ni 142 na upungufu ulikuwa ni madarasa 110. Hivyo kupitia kukamilika kwa ujenzi wa vyumba 110 vinaenda utakidhi mahitaji ya wanafunzi wote waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023.
Sera ya Elimu na mafunzo ya mwaka 2014 inalenga kuwa na mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia ambapo serikali inatamka katika kifungu 3.2.12. kuwa itahakikisha kuwepo kwa miundombinu bora na stahiki ya kutosheleza mahitaji ya elimu na mafunzo kwa makundi yote katika ngazi zote za elimu na mafunzo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.