Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Bi Ummy Wayayu amewataka wanamichezo watumishi wanaoshiriki mashindano ya michezo ya shirikisho la michezo serikali za mitaa Tanzania (SHIMISEMITA) kuhakikisha wanarudi na ushindi mkubwa Ilemela
Ametoa rai hiyo tarehe 29 Agosti 2024 alipofika kuwajulia hali na watumishi hao yanayoendelea katika chuo cha ualimu Butimba Mwanza ambapo alitumia fursa hiyo kuwapongeza kwa kuaminika na kuchaguliwa kuiwakilisha Ilemela katika mashindano hayo huku akiwaahidi donge nono pindi watakaporudi na ushindi Ilemela
Nao viongozi wa timu zinazoiwakilisha halmashauri ya manispaa ya Ilemela katika (SHIMISEMITA) kwa niaba ya wanamichezo hao wameahidi kutwaa ubingwa wa mashindano hayo na kurudi na ushindi nyumbani kwa kuzishinda timu zote za maeneo mengine watakazoshindana nazo.
Nahodha wa kikosi cha timu ya mpira wa miguu wanaume cha manispaa ya Ilemela Mwalimu Harith Hamis kutoka shule ya msingi Kilimahewa amesema kuwa timu yake haikuja kushiriki tu mashindano hayo badala yake wamekuja kuchukua ushindi kwani kikosi chao kipo vizuri na kuwataka wapinzani wao kujipanga haswa ili kuikabili timu hiyo vinginevyo watakuwa wamekuja Mwanza kutalii badala ya kushiriki mashindano hayo
Mwalimu Joyce Hepas Mwara kutoka shule ya msingi Gedeli ni nahodha wa timu ya fani za ndani itakayoshiriki mashindano ya kwaya ambapo amefafanua kuwa ili kauli mbiu ya wilaya hiyo iweze kuwa na maana ya ‘Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’ ni lazima wapenzi na mashabiki wajitokeze kwa wingi ili kujionea ubora na ufundi wa kikosi chake kwani wamejipanga kutoa burudani na kurudi na ushindi katika mashindano hayo
Afisa utamaduni kutoka Ilemela Bi Lulu Ndari amesema kuwa timu za wilaya yake zimejiandaa vizuri kwani zilifanya mazoezi ya kutosha na kwamba zinaendelea kushiriki michezo yote ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa wavu, mpira wa pete, kuvuta kamba na kwaya huku akiwataka watumishi wa Ilemela kujitokeza kuiunga mkono na kuishabikia ili iweze kupata morali na ari ya kufanya vizuri zaidi wakati wote wa mashindano
Mashindano ya SHIMISEMITA yanaendelea kurindima katika viwanja mbalimbali vya chuo cha ualimu Butimba na Magereza jijini Mwanza yakishirikisha timu zaidi ya 50 kutoka halmashauri za manispaa, halmashauri za wilaya, halmashauri za miji midogo na majiji yakisindikizwa na kauli mbiu isemayo, “Shiriki uchaguzi wa serikali za mitaa kwa maendeleo endelevu”
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.