Na Paschalia George, Ilemela
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary ambae pia ni mwenyekiti wa kamati ya Mpango wa kitaifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA) katika Manispaa ya Ilemela amewataka wazazi kuona thamani ya watoto wao kwa kutenga muda wa kuwa nao karibu kipindi cha makuzi yao na kuwapa malezi bora.
“Wazazi tumekuwa hatuna muda wa kukaa na watoto wetu kwa kisingizio cha kutafuta pesa,tutenge muda wa kuongea na watoto mara kwa mara ,tuache kupeleka watoto wadogo shule za bweni kwani bado wanahitaji malezi ya mzazi kwa karibu, amesema
Mhandisi Modest ameyasema hayo katika kikao cha kujadili mikakati mbalimbali ya namna ya kutokomeza ukatili wa kijinsia huku akisisitiza suala la kuendelea kutoa elimu katika maeneo yote ndani ya Ilemela, maeneo ya mikutano , ibada,shuleni mikutano ya hadhara sambamba na elimu za uelewa wa kawaida ndani ya kaya.
Katika nyakati tofauti, wawakilishi wa viongozi wa dini Ilemela wameendelea kukemea vitendo vyote vya kikatili vinavyotendwa kwa kina mama na watoto na kuitaka jamii kuacha mara moja kwani ni kinyume cha maadili ya imani zetu za dini.
“Hatutaacha kukemea vitendo hivi kwani nasi tunatambua tunayo nafasi kubwa katika kupaza sauti zetu kwa waumini wetu katika nyumba za ibada.Vitendo vya ulawiti vimekithiri sana katika jamii yetu ni tamaduni mpya ambayo wakati mwingine hata sisi viongozi wa dini tunaumia sana kuona jamii tena watoto kujihusisha katika uchafu huu.” amesema Shekhe Sululu Salum mwakilishi wa viongozi wa dini ya Kiislam Ilemela.
Nae mwakilishi wa madhehebu ya kikristo Ilemela mchungaji Robert Bundala amesema “Tunaungana na jamii ya Ilemela katika kutokomeza kabisa vitendo vya unyanyasaji japo tunatambua hata katika dini zetu wapo watu wanaohubiri mafundisho potofu na wakati mwingine viongozi haohao wa dini kuwa vinara katika kufanya ukatili huu kupitia imani zetu.Sisi viongozi wa dini tutaongea kwa nafasi yetu.
Kamanda wa polisi Wilaya ya Ilemela Elisante Ulomi ameitaka jamii ya Ilemela kupaza sauti juu ya matukio yote ya unyanyasaji yanayojitokeza ndani ya jamii
“Msiogope sisi vyombo tupo kwa ajili ya kuwalinda raia na mali zenu,kufichiana siri na kuogopana ni kuongeza tatizo ndani ya jamii yetu.Tusimame imara kutetea mama zetu,mabinti zetu,watoto wetu na jamii kwa ujumla, amesisitiza hilo.
Manispaa ya Ilemela imeendelea kusimamia na kufuatilia kwa karibu shughuli za Mpango wa kitaifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kwa kutambua kuwa wanawake na watoto ndio kundi waathirika zaidi na vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kuliko makundi mengine ndani ya jamii.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.