“Tutumie gesi badala ya mkaa,tubadilike na tuache mazoea”Ni kauli yake Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela John Wanga alipomuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongela katika kilele cha maadhimisho ya siku ya mazingira duniani.
Akihutubia wananchi waliofika katika maadhimisho ya siku ya mazingira duniani yaliyoambatana na kauli mbiu isemayo, Mkaa ni gharama, tumia nishati mbadala, amewaasa wananchi kuacha kukata miti hovyo na kufuata sheria za nchi na kuwataka kufika ofisi ya Mkurugenzi kwa ajili ya kupata kibali pindi wanapotaka kukata miti.
“Unapotaka kukata mti unatakiwa kufika ofisi ya Mkurugenzi kwa ajili ya kupata kibali”, alisema Mkurugenzi.
Aidha amewataka wananchi kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha kuwa wanatunza mazingira kwa kuacha kukata miti hovyo, kuepuka ujenzi holela kwa kufuata sheria za mipangomiji pamoja na kuacha ufugaji holela maeneo ya mjini.
Maadhimisho haya yameenda sambamba na upandaji wa miti ya miembe huku Mkurugenzi akiwataka viongozi wa kata kuhakikisha kuwa miti hiyo inatunzwa ambapo alitoa ufafanuzi kuwa miti iliyopandwa katika maeneo ya watu itunzwe na wahusika wa maeneo hayo na ile iliyopandwa katika maeneo ya wazi ni jukumu lao viongozi kuitunza.
Halikadhalika kupitia kauli mbiu ya siku hii, Mkaa ni gharama, Tumia nishati mbadala amewahimiza wananchi kuzingatia matumizi ya nishati mbadala na suala la usafi wa mazingira.
Nae Diwani wa kata ya Kawekamo ambapo kilele cha maadhimisho ya siku hii yamefanyika, Mhe.Japhes Rwehumbiza ameushukuru mkoa kwa kuhitimishia katika kata yake huku akisisitiza ufikishwaji wa elimu ya matumizi ya nishati mbadala ngazi ya mitaa na kuwa elimu hiyo isiishie katika mabango tu kwani wananchi wengi hawana elimu ya kutosha juu ya nishati mbadala.
“Elimu ya nishati mbadala haijafika kwa wananchi,isiishie kwenye mabango bali ishuke hadi ngazi ya kata”, alisema alipokuwa akimkaribisha mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa Ndugu John Wanga kwa ajili ya kuhitimisha maadhimisho hayo.
Nae Afisa Mazingira wa Manispaa ya Ilemela Ndugu Simon Nzagi amesema kuwa, kauli mbiu hii imekuja kwa muda muafaka na kuwa ina mapana zaidi ya watu wanavyoifikiria na kuwataka wananchi kutumia nishati hizi kwa busara ili kuweza kuhifadhi miti ambapo ikikatwa hovyoo inaweza kusababisha jangwa,ukosefu wa mvua, kupotea kwa wanyama na hatimae kusababisha uchumi wa nchi kushuka.
Ndugu Emmanuel Lufunga ambae ni mmoja wa wananchi waliohudhuria kilele cha maadhimisho hayo ameiomba serikali kuwa maadhimisho haya yasiishie tu mjini bali yafike na vijijini huku akisisitiza utoaji wa elimu ya nishati mbadala.
Kila mwaka ya tarehe 05 mwezi wa sita dunia huadhimisha siku ya mazingira, madhumuni ya maadhimisho ya siku hii ni kutoa fursa ya kukuza uelewa wa jamii kuhusu masuala mbalimbali ya mazingira na kuhamasisha jamii kuchukua hatua za makusudi za kuhifadhi mazingira kwa ustawi wa sasa na maisha ya baadae.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.