Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela , John Wanga, ambae pia ni Afisa Mwandikishaji wa jimbo la Ilemela leo amefungua rasmi mafunzo ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga Kura kwa watendaji wa kata ambao wanafahamika kama maafisa waandikishaji wasaidizi ngazi ya Kata yatakayochukua siku mbili za tarehe 06-07/8/2019.
Akifungua Mafunzo hayo, Mkurugenzi amewataka waandikishaji wasaidizi ngazi ya kata kuhakikisha wanafuatilia na kusikiliza mafunzo haya kwa umakini kwani kazi hii ya uboreshaji wa dafatri ni nyeti na ni kwa maslahi ya maendeleo ya nchi.
Mafunzo haya yanayotolewa na waandikishaji wasaidizi ngazi ya jimbo yanahusisha mfumo mzima wa namna ya zoezi zima la uandikishaji ambapo mfumo huu umegawanyika katika maeneo matatu ambayo ni uandikishaji wa mwananchi mpya kabisa, uboreshaji wa taarifa za mpiga kura kwenye daftari (hii ni iwapo mwannachi alihama eneo la makazi au iwapo taarifa zilikosewa)pamoja na kumuondoa mpiga kura kwenye daftari kutokana na sababu mbalimbali kama vile kifo.
Mafunzo haya pia yamehusisha kuapishwa kwa waandikishaji wasaidizi ngazi ya kata, namna ya ujazaji wa fomu mbalimbali pamoja na namna ya kutumia sanduku linaotumika kubeba vifaa mbalimbali ambavyo vimeunganishwa na kufanya kazi pamoja kwa ajili ya kuingiza taarifa binafsi za mpiga kura ( BVR KIT-Biometric Voters Registration Kit)
Mara baada ya kukamilika kwa mafunzo haya, mafunzo yatakayofuatiwa yatatolewa kwa mtendaji ambae atahusika na uingizaji wa taarifa za wapiga kura katika mfumo wa kuandikisha wapiga kura(BVR Kit operator) pamoja na waandikishaji wasaidizi ambayo yatafanyika kwa siku 2 za tarehe 10-11/08/2019.
Zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura katika jimbo la Ilemela litaanza rasmi mnamo tarehe 13/08/2019 na litadumu kwa muda wa siku 7 hivyo kukamilika siku ya tarehe 19/8/2019 na zoezi hili litaendeshwa katika kata zote 19 za Manispaa ya Ilemela.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.