MKURUGENZI AWAHIMIZA WAATHIRIKA WA MADAWA YA KULEVYA KUZINGATIA MASHARTI.
Mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Ndugu John Wanga amewahimiza watumiaji wa madawa ya kulevya kufuata masharti wanayopewa na wataalam wa vituo vya urejeshaji hali na udhibiti wa matumizi ya madawa ya kulevya ili kujenga taifa lenye nguvu na maendeleo.
Hayo yalisemwa na afisa maendeleo ya jamii wa manispaa ya Ilemela Bi Sarah Nthangu ambae alimwakilisha mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa hiyo, wakati akikabidhi msaada wa mahitaji ya kila siku katika kituo cha Back to life Sober House kilichopo Lumala kata ya Ilemela.
“Mkurugenzi wetu anatupenda na ameamua kuonyesha upendo wake kwa kutuletea vitu hivi kuonyesha kuwa yupo pamoja nanyi kwa siku hizi mtakazoendelea kuwa hapa na kuwa msijisikie upweke, mmetengwa au mmetupwa, Lakini pia anasisitiza kuwa tufuate masharti ambayo tunapewa ili turudi katika hali zetu za kawaida kwasababu taifa linatutegemea sana na linaumia kuona tunaingia katika hii hali”, alisema
Aidha Bi sara aliongeza kwa kusema kuwa vita dhidi ya madawa ya kulevya si ya serikali peke yake bali ni ya jamii yote hivyo aliitaka jamii kumuunga mkono Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhidi ya mapambano hayo kwa maslahi mapana ya taifa letu.
Nao waathirika wa madawa hayo kutoka katika kiituo hicho wakiwakilishwa na Ndugu Ally Athumani kwa niaba ya msimamizi wa kituo mbali na kumshukuru Mkurugenzi wa Ilemela kwa msaada huo wameitaka Serikali kuanzisha vituo vya urejeshaji hali kwa watumiaji wengine wa maeneo mbalimbali nchini na kuongeza kasi ya upambanaji wa vita dhidi ya uingizaji na matumizi ya madawa ya kulevya nchini ili kupunguza idadi ya wahanga wa madawa hayo na nguvu kazi kwa taifa.
Msaada uliotolewa katika kituo hicho ni pamoja na mchele kilo mia moja, mafuta ya kupikia lita Ishirini, mafuta ya kupakaa, sabuni za kuogea na kufulia, maharage kilogram 50, sukari kilogram Ishirini na tano na chumvi vitu hivyo viligharimu kiasi cha Tshs 500,000 tu.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.