Mhandisi Modest Apolinary Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela amesisitiza suala la ushirikiano ili kuweza kufikia malengo yaliyowekwa kwani mawazo ya wengi hutoa majibu mengi.
“Ushirikiano wetu utatufikisha tunapopataka, kwani ni vizuri kufanya kazi kwa kushirikiana na mawazo ya wengi hutoa majibu mengi”,alisema
Ameyasema hayo alipotembelea eneo la soko la Bujingwa, alipokuwa katika ziara ya kikazi ya ukaguzi wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika kata ya Buswelu.
Pamoja na hayo amesisitiza suala la kutokuruhusu migogoro ya mipaka ya ardhi kuturudisha nyuma kimaendeleo hasa katika maeneo ya shule kwa kutambua kuwa shule ni muhimu kwa watoto.
“Tusiruhusu migogoro ya mipaka ya ardhi iturudishe nyuma kimaendeleo,tunatambua kwamba shule ni muhimu kwa watoto wetu”, alisisitiza.
Mhe.Sara Ng’wani, ambae ni diwani wa kata ya Buswelu alitumia ziara hiyo kumueleza mkurugenzi suala la ukamilishaji wa ujenzi wa daraja ambalo linatenganisha kata ya Kiseke na Buswelu kwani limekuwa likileta maafa kutokana na ubovu wa daraja hilo.
Pamoja na hayo alishukuru kwa kuanza kwa ujenzi wa shule ya msingi kwa nguvu za wananchi lakini pia kufufua soko la Bujingwa kwani litaleta nafuu ya maisha kwa wakazi wa hapa, amesema Mhe Sarah
Akijibu changamoto hizo zilizotolewa na Mhe.Sarah, Mkurugenzi amesema hakuna changamoto zisizo na utatuzi ni suala la kukaa pamoja kuelekezana na kueleweshana na kupata muafaka wenye tija.
Kuhusu suala la maboresho ya soko na ombi la ujenzi wa zahanati eneo lililokuwa josho la mifugo ameshauri kuwa iandaliwe michoro na bajeti yake ili kuweza kuona tunajipangaje kukamilisha hili ikibidi hata kuwashirikisha wadau mbalimbali kwani lengo letu ni kufanikisha.’’ Alisema
Miongoni mwa maeneo yaliyotembelewa ni ujenzi wa shule mpya ya msingi Bujingwa, eneo la josho Bujingwa,soko la Bujingwa,baadhi ya maeneo yanayostahili kulipwa fidia eneo la mbogamboga barabara ya Buswelu – Nyamadoke .
Mkurugenzi ameendelea na ziara za kawaida kwa ajili ya kutambua maeneo na miradi mbalimbali inayotekelezwa ndani ya manispaa ya Ilemela sambamba na kufuatilia mienendo ya utekelezaji wa majibu ya kero mbalimbali za wananchi zinazoendelea kupokelewa na kujibiwa.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.