Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary amewataka watendaji wa kata kuhakikisha kuwa wanausimamia kiukamilifu mkataba wa lishe waliosaini wito huo umetolewa wakati wa zoezi la kusaini mkataba huo
Akifafanua maana ya kusaini mkataba huo, Mhandisi Modest amesema kuwa ni kuhakikisha udumavu unakwisha kabisa katika Manispaa ya Ilemela kwa kuwafuatilia wakinamama na kuhakikisha kuwa wanafuata taratibu zote za lishe ambapo amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2022/2023 Ilemela imetenga kiasi cha Shilingi milioni 88 kwa ajili ya utekelezaji wa afua za lishe.
“Maana ya kusaini hii mikataba kwenye ngazi za chini ni kuhakikisha wakina mama wanafuata taratibu zote na kama kwenye mtaa kuna mama ana mtoto mwenye unyafuzi taarifa iwasilishwe ili wapate chakula chenye virutubisho pamoja na kuwafundisha kuandaa chakula, haya ni maelekezo ya Mhe Rais hivyo kila mmoja akawajibike kwa hilo”, amesema Mhandisi Modest
Aidha ameongeza kusema kuwa kupitia bajeti ya mwaka 2022/2023 ya Ilemela iliyotengwa kwa ajili ya masuala ya lishe ameelekeza kuwa asilimia 60 ya fedha hizo zikasaidie watoto wenye unyafuzi wa hali ya juu na fedha zisilipe posho bali zikatumike kununua vyakula vya lishe na tiba kwa ajili ya watoto hao ili Ilemela ifute kabisa unyafuzi.
Nao watendaji wa kata kupitia mwakilishi wao ndugu Mponeja katemi, mtendaji wa kata ya Kayenze wameahidi kwenda kuutekeleza mkataba wa lishe kama ambavyo mhe Rais ameelekeza huku wakitambua kwamba rasilimali za kuetekeleza mkataba huu zipo ndani ya jamii zetu kwa kushirikiana na Halmashauri kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023
Paulina Machango ambae ni afisa lishe wa Manispaa ametoa rai kwa watendaji wa kata kuhakikisha kuwa wanawatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambao wamewezeshwa kufanya kazi katika jamii katika kutoa elimu ya lishe kwa wajawazito, wanaonyonyesha na wazazi au walezi wa watoto chini ya miaka mitano
Mkataba huo wa lishe unalenga kuhakikisha kuwa hali ya lishe inaboreka pamoja na kupunguza atahari za utapiamlo katika jamii. Sambamba na kuhakikisha kuwa jamii kupitia uongozi wa kata inashiriki ipasavyo katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa mpango wa halmashauri na afua za lishe.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.