Mkandarasi M/S China Railway 15 Bureau Group Cooperation kutoka nchini China atakaetekeleza mradi wa ujenzi wa soko la kirumba na barabara zake zenye urefu wa km 2.9 kwa gharama ya shilingi za kitanzania bilioni 14.71 (bila VAT) amekabidhiwa rasmi eneo la kazi kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kumkabidhi mkandarasi eneo la kazi iliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya kata ya kirumba litakapojengwa soko hilo siku ya tarehe 14 Novemba 2024, mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu matumizi ya fedha na kuhakikisha mradi huu unatekelezwa Ilemela, pamoja na hayo amemtaka mkandarasi kutumia wazawa kwa kazi zisizohitaji utaalam mkubwa.
“Katika siku niliisubiria kwa hamu ni hii ya leo tunapo mkabidhi mkandarasi eneo kwa ajili ya kazi, maneno yalikuwa mengi lakini leo tunashuhudia kazi inaenda kuanza, tumshukuru sana Rais Dkt Samia”. Alisema Mbunge
Aidha Mhe Mabula amewataka wananchi wanaoishi jirani na mradi huo kutanguliza maslahi ya umma mbele kwa kutoa ushirikiano kwa mkandarasi pamoja na kulinda mali na vifaa vyote vitakavyoletwa kwaajili ya ujenzi wa mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati
Kwa upande wake meneja wa wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA mhandisi Sobe Makonyo mbali na kumshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa kutoa fedha za ujenzi wa mradi huo akaongeza kuwa kazi zitakazotekelezwa na mkandarasi ni ujenzi wa soko la kisasa na ujenzi wa barabara zenye urefu wa km 2.9 huku akiahidi kumsimamia mkandarasi ili tija ya mradi huo iweze kufikiwa
Shabani kasiaga ni mwakilishi wa kampuni ya ms china railway 15 bureau group cooperation ambapo ameahidi kufuata miongozo yote iliyopo kwenye mkataba wa ujenzi wa mradi huo huku akiwaomba wananchi na viongozi kutoa ushirikiano wakati wote wa utekelezaji wa mradi huo ili waweze kuukamilisha kwa wakati na ubora unaohitajika
Nusura Abdalla Omary na Bakari Said ni wananchi wa kata ya Kirumba na wafanyabiashara wa soko la zamani katika kata hiyo wao wamepongeza na kuishukuru serikali kwa hatua iliyofikiwa ya kuhakikisha soko hilo la kisasa linajengwa sambamba na kumtaka mkandaraasi kuhakikisha soko jipya litakapokamilika hakutakuwepo na changamoto ya maji kujaa ndani ya soko kama ilivyokuwa hapo zamani.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.