Mnamo tarehe 17/11/2017, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela alifanya ziara katika kata ya Bugogwa kwa ajili ya kusikiliza kero mbalimbali za wananchi halikadhalika kuelezea wananchi mipango ya halmashauri katika kuwaletea maendeleo.
Akizungumza na wananchi wa kata hiyo aliitaja miradi mbalimbali inayoendelea pamoja na shughuli zinazoendelea kutekelezwa katika kata ya Bugogwa ikiwemo zoezi la urasimishaji makazi, ujenzi wa majengo ya zahanati ya Karume katika kuhakikisha huduma za afya na huduma za mama na mtoto zinaimarika pamoja na mradi mkubwa wa usambazaji maji unaoendelea na kuwafafanulia juu ya hatma ya mradi wa umeme wa vijijini REA unaoendelea kutekelezwa katika vijiji vya kata hiyo.
Aidha aliwataka wananchi kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Daktari John Magufuli, Mbunge wa jimbo la Ilemela mheshimiwa Daktari Angeline Mabula na madiwani katika usimamizi wa miradi mbalimbali inayoendelea ili kuweza kufanikisha ukamilikaji wa miradi hiyo.
Pamoja na hayo aliahidi mifuko ya Saruji na Nondo kwa ajili ya ujenzi wa daraja kwa wananchi wa mtaa Igombe B iwapo nao watachangia mawe ya ujenzi wa daraja hilo.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Bugogwa mheshimiwa William Mashamaba mbali na kuishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa utekelezaji wa miradi hiyo ya maendeleo katika kata yake amewahakikishia ushirikiano katika kuhakikisha inafanikiwa tena kwa wakati huku akiwataka wananchi wake kufuata sheria na taratibu ili kujiepusha na usumbufu usiokuwa wa lazima.
Akihitimisha mkutano wa ziara hiyo Mstahiki Meya wa manispaa ya Ilemela ambae pia ni diwani wa kata Sangabuye mheshimiwa Renatus Mulunga amewakumbusha wananchi hao juu ya umuhimu wa kuchangia shughuli za maendeleo ikiwemo utaratibu wa manispaa yake wa kusaidia kumalizia miradi inayoanzishwa na wananchi wenyewe huku akitolea mfano wa kuezekwa kwa msaada wa manispaa kwa jengo litakalokuwa limefikia hatua ya boma litakalojengwa kwa nguvu za wananchi.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.