Jumla ya mitaa kumi na tano ikiwemo Butindo, Chabakima, Ibaya, Bulyang'hulu, Mwakalundi, Masemele, Igogwe, Kimanilwentemi, Nkoronto, Isanzu, Bujingwa, Nyashimba, Bujimile na Nyanguku inayopatikana Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza inatarajiwa kunufaika na mpango wa usambazaji umeme vijijini REA .
Hayo yamesemwa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe. Dkt.Angeline Mabula wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi na kutoa mrejesho wa mipango ya maendeleo itakayotekelezwa na Serikali baada ya kuisha kwa vikao vya bunge la bajeti katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika viwanja vya Winter fall kata ya Nyasaka ambapo amefafanua kuwa licha ya Ilemela kuwa manispaa bado itanufaika na mpango wa usambazaji umeme vijijini kwa kuwa baadhi ya maeneo bado yana sura ya vijiji.
'.. Ilemela ina sura ya kijiji, na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hasan akaliona hilo na ameridhia na sisi tupate umeme wa REA, Tumshukuru sana Rais wetu ..' Alisema
Aidha Dkt. Mabula akaongeza kuwa manispaa ya Ilemela kupitia mapato yake ya ndani inao mpango wa kujenga kituo kipya cha afya chenye thamani ya zaidi ya milioni 250 katika kata ya Ibungilo.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Nyasaka Mhe. AbdulRahman Simba ameishukuru Serikali kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya kata yake ikiwemo milioni mia mbili zilizotumika kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na madawati katika shule ya sekondari Nyasaka, milioni 38 ujenzi wa daraja la Nyamuge, milioni 880 ujenzi wa barabara ya mawe ya Kiloleli 'B' yenye urefu wa km 1.3 na milioni 130 kwaajili ya ujenzi wa barabara ya Chamwenda sanjari na kumpongeza Mbunge wa Jimbo hilo kwa namna anavyoshirikiana nae.
Nae afisa mipango miji wa Manispaa ya Ilemela Chigulu Kennedy amewataka wananchi kufuatilia hati za malipo za upimaji shirikishi Ili waweze kumilikishwa viwanja vyao pamoja na kuahidi kuyasimamia makampuni yote yanayofanya upimaji ndani ya manispaa ya Ilemela ili wananchi waweze kupimiwa kwa wakati na kumilikishwa .
Daud Chitongolo na Bi. Fatna Swalehe ni wakazi wa kata ya Nyasaka Kwa nyakati tofauti wamelalamikia uvamizi wa mipaka katika maeneo yao na zoezi la upimaji shirikishi kuchelewa hivyo kuiomba Serikali kuyafuatilia makampuni yaliyofanya kazi hiyo katika maeneo yao kwa ajili ya ufumbuzi wa kero zao.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.