Halmashauri ya Misenyi na Misungwi zimezuru manispaa ya Ilemela kujifunza namna manispaa hiyo inavyotekeleza shughuli zake za kimaendeleo hasa katika masuala yanayohusu mipango miji, mapato na utekelezaji wa miradi na mipango yake
Ziara hiyo imejumuisha wataalamu wa halmashauri hizo na madiwani wake ikiongozwa na mwenyekiti wa Misenyi mheshimiwa Projestus Tegamaisho na mkurugenzi wake Limbe Bernald ambapo mbali na kufurahishwa na mapokezi mazuri amesema kuwa lengo la ziara ni kujifunza namna Ilemela inavyofanya shughuli zake sambamba na kuimarisha uhusiano baina ya pande hizo mbili kwa lengo la kuboresha utoaji huduma na kuleta maendeleo huku wakitumia gharama nafuu
‘… Ilikuwa ni ghafla lakini kwa bahati nzuri mmetupokea vizuri na kutupatia ushirikiano mkubwa, Lengo la ziara yetu ni kujifunza namna mnavyotekeleza shughuli zenu za kimaendeleo hasa kwenye mapato, mipango miji, miradi na mipango kama tulivyoona huu uzio wenu imara, bora na wakisasa tumesikia kuwa mmetengeneza kwa fedha za mapato ya ndani na kwa gharama nafuu hii inatufanya kujifunza namna mnavyosimamia mapato yenu ...’ alisisitiza
Aidha ziara hiyo ilihusisha matembezi ya baadhi ya miradi inayotekelezwa na Ilemela ikiwemo mradi wa bweni la wasichana la shule ya sekondari Buswelu, mradi wa ujenzi wa madarasa ya shule ya msingi Buswelu na mwalo wa soko la kirumba vikitanguliwa na kikao cha pamoja cha wataalamu wa manispaa hizo na madiwani wake
Kwa upande wake mwakilishi wa Meya wa manispaa Ilemela ambae pia ni diwani wa kata ya Buswelu yalipo makao makuu ya wilaya mheshimiwa Sarah Ng’wani ameshukuru kutembelewa na ugeni huo huku akitaka kuimarishwa kwa mahusiano ya pande hizo
‘…Ili tubadilishane mawazo wewe mwenzangu unafanyaje ni lazima tukae pamoja wataalamu wetu wamejipanga vizuri mjifunze na kupata picha halisi ya kinachotendeka ili kama kuna pahala mnakosea au tunakosea kwa pamoja tuweze kufanikisha …’ alisema
Akihitimisha mkurugenzi wa manispaa Ilemela ndugu John Wanga amezikaribisha pia manispaa nyengine kuja kujifunza na kuwahakikishia kuwa pamoja na upya wake Ilemela itaendelea kuwa manispaa ya mfano na kuigwa katika utekelezaji wa shughuli za kimaendeleo
‘… Ilemela ni manispaa mpya tunawakaribisha sana kujifunza iwe shughuli zetu za ndani au za nje …’ alihitimisha
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.