Kiasi cha shilingi milioni 739 kimetumika kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya kata ya Nyamanoro jimbo la Ilemela ikiwemo miradi ya elimu, afya na miundo mbinu ya barabara.
Hayo yamebainishwa na mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe. Dkt. Angeline Mabula wakati wa muendelezo wa ziara yake jimboni kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi, kukagua miradi ya maendeleo na kuhamasisha ushiriki wa uchaguzi wa serikali za mtaa, kujiandikisha katika daftari la mkaazi na kilele cha mbio za Mwenge katika viwanja vya mtaa wa Mnyapala ambapo amewataka wananchi wa kata hiyo kumpongeza na kumshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo za miradi.
".. Tuna kila sababu ya kusema ahsante Dkt. Samia, ametoa fedha nyingi sana kufanikisha miradi ya maendeleo, Ilemela kama jimbo tumeendelea kunufaika na fedha za miradi mbalimbali na hata nyie Nyamanoro mmenufaika pia, miradi mikubwa inaendelea kutekelezwa, barabara nyingi zinaendelea kufunguliwa ndani ya kata yenu .." Alisema
Aidha Mhe.Mabula ameongeza kuwa serikali ya awamu ya sita imeendelea na kasi ya kukamilisha miradi mikubwa na ya kimkakati ikiwemo reli ya mwendo kasi na kisasa ya SGR, daraja la Busisi, meli kubwa za MV Mwanza Hapa Kazi Tu, upanuzi wa uwanja wa ndege Mwanza na miradi mikubwa ya maji hivyo kuwaasa wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali ili kuharakisha maendeleo.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Nyamanoro Mhe.George Maganiko Ngaka mbali na kuishukuru serikali kwa fedha za miradi ya maendeleo amempongeza mbunge huyo kwa kuchochea shughuli za maendeleo ndani ya kata yake pamoja na kuahidi kuendelea kushirikiana nae ili kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Jeremiah Lugembe ni mwakilishi wa mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela amesema manispaa ya Ilemela itaendelea kutenga fedha za mapato ya ndani na serikali kuu kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ndani ya kata hiyo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na kutatua kero za wananchi .
Joachim Elias na Anna Samuel ni wananchi wa kata ya Nyamanoro kwa nyakati tofauti wameishukuru Serikali kwa kutekeleza miradi mingi ndani ya kata yao .
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.