Uwezeshaji wa wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi ni sehemu ya Dira ya maendeleo ya Taifa kufikia mwaka 2025 ambapo sehemu kubwa ya uchumi wa Tanzania inatarajiwa kumilikiwa na watanzania wenyewe iwapo maendeleo hayo yatajumuisha watanzania wote pamoja na kutoa nafasi kwa makundi yote kujiendeleza kikamilifu hasa yale makundi yenye uwezo mdogo.
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kutoka sekta binafsi imekuwa ikitekeleza majukumu mbalimbali ya kuwawezesha wananchi kiuchumi. Ili uwezeshaji wa wananchi kufanyika kwa ufanisi na kumuwezesha mtanzania kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kumiliki rasilimali.
Kila Mamlaka za Serikali za Mitaa Tanzania, zinao wajibu wa kutenga asilimia kumi ya mapato yanayokusanywa kutoka kwenye vyanzo vya ndani vya mapato kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vilivyosajiliwa vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu hii ni kwa mujibu wa kanuni 4.-(1) ya Kanuni Za Utoaji Na Usimamizi wa Mikopo Kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana Na Watu Wenye Ulemavu.
Awali fedha hizo za mkopo kwa makundi hayo mawili zilikuwa zikitolewa kwa masharti ya riba, ya asilimia 10 kwa mwaka na kufikia mwaka 2017 serikali iliziagiza mamlaka za serikali za mitaa kuongeza kundi la walemavu.
Ili kuweza kuwasaidia wanawake, vijana na walemavu kujikwamua kiuchumi, mwaka 2018 serikali iliamua kuwa mikopo hiyo itolewe bila riba ili kuwapa fursa wanawake, vijana na walemavu kwa ajili ya kuanzisha miradi kwa wingi ya kujikwamua kiuchumi kwani suala la riba limekuwa kikwazo kwa makundi mengi kuweza kukopa na kurejesha mikopo kwa wakati
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ni miongoni mwa Halmashauri ambayo imekuwa ikitoa mikopo hiyo tangu ilipoanzishwa mnamo mwaka 2012, ambapo ilianza kutoa mikopo kwa makundi ya wanawake na vijana kupitia kamati ndogo za mikopo zilizoundwa katika ngazi ya kata na kuratibiwa na maafisa maendeleo ya Jamii wa kata na kupitishwa na kamati za Maendeleo za kata (WDC) na kisha kupitishwa katika vikao vya kamati za kudumu za Halmashauri.
Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imeendelea kutekeleza agizo hilo kwa kutenga asilimia 10 kutoka katika vyanzo vya mapato ya ndani pamoja na kutoa mikopo hiyo kwa wanawake, vijana na walemavu.Ambapo asilimia 4 ya mapato ya ndani huelekezwa kwa wanawake, asilimia 4 kwa ajili ya vijana na asilimia 2 hupewa watu wenye ulemavu.
Ili kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika kwa malengo tarajiwa, wataalamu kutoka idara ya maendeleo ya jamii ya Manispaa ya Ilemela kwa kushirikiana na madiwani wa viti maalum, huhakikisha kwanza wanawajengea uwezo kwa kuwapa elimu na mafunzo mbalimbali juu ya matumizi sahihi ya fedha hizo.
Vikundi vingi vinavyopatiwa mikopo hiyo hujishughulisha na shughuli za ushonaji, utengenezaji wa batiki,sabuni za maji, kilimo cha bustani., biashara ya dagaa na samaki , ufugaji na shughuli za uchomeleaji
Kikundi cha vijana kinachojulikana kama mafundi welding ni mojawapo ya kikundi kinachofaidika na mkopo huu kutoka Halmashauri kilichopo Kata ya kirumba na hujishughulisha na shughuli za kutengeneza milango, madirisha pamoja na nanga za vyombo vya majini
Alex Stephen ambae ni katibu wa kikundi cha vijana mafundi welding anaeleza kuwa mkopo huu umewasaidia sana kwani walianza na mtaji wa kiasi cha shilingi laki tano lakini hadi kufikia sasa mtaji wao umefikia kiasi cha Shilingi Milioni tatu za kitanzania.
“Tulianza kazi zetu kwa kusuasua, kwa mtaji mdogo wa mashine moja ya thamani ya shilingi laki tano, ambayo wote tulikuwa tunaitegemea katika kufanya kazi ambapo ilitulazimu kusubiriana lakini baada ya kupata mkopo awamu ya kwanza wa kiasi cha shilingi milioni mbili mambo yalibadilika.”Alisema
Aliendelea kusema kuwa, mkopo huu umewafanya kupiga hatua moja kwenda nyingine mpaka sasa wana jumla ya mtaji wa shilingi milioni tatu na wanazo mashine nne za kuchomelea tofauti na awali walikuwa nayo moja tu hivyo kusababisha kuchelewesha kazi za wateja wao.
Aidha aliishukuru serikali ya kata kwa kuunga mkono shughuli zao mfano zinapotokea zabuni hushirikishwa huku akitoa ushuhuda kuwa wamepewa kazi ya kutengeneza madirisha ya shule ya sekondari Kirumba hii ni moja ya hatua mpaka sasa.
Huku akiishauri Serikali kuwa ijitahidi kuendelea kutoa kipaumbele kwa vijana kwasababu mwamko na morali wa kufanya kazi upo kwani wakiwezeshwa zaidi wataweza kufanya makubwa zaidi ya hapa huku wakigusia changamoto kubwa waliyonayo ya eneo na kuomba kupatiwa eneo ili kuwarahishia kazi zao.
Nae Bi Veronica Pole Mwenyekiti Msaidizi wa kikundi cha wakinamama malengo kutoka kata ya Buswelu alisema kuwa kikundi chao hujishughulisha na ujasiriamali wa Biashara ya kuuza pochi, vikapu na sabuni kwa matumizi ya nyumbani ambapo husambaza ndani ya Mwanza na nje ya Mwanza.
Alisema kuwa walianza na mtaji wa kiasi cha shilingi laki nane na kufanikiwa kununua vifaa vyote lakini ambapo hadi sasa wamefikisha mtaji wa milioni mbili tofauti ambayo ni tofauti na mkopo wanaopata hivyo ukiweka na halmashauri mtaji umekuwa na kufikia shilingi milioni nane.
“Tunaishukuru halmashauri ilitukopesha milioni mbili laki tano tukarejesha ikatuongezea tena milioni nne na wenyewe tumeweza kuurejesha, mara ya kwanza tulikuwa tunarejesha kwa riba lakini sasa hivi hatulipi riba, Kwa ushauri kwa mkopo tunaomba watuongezee tutakapoomba tena mkopo ili tupate kikubwa zaidi maana tunampango wa kufungua biashara kubwa zaidi tunataka tuwe wakala wa mpesa na mabenki ili tuwe na mradi mwengine”, Alisema.
Kupitia mkopo wa halmashauri tumeweza kukuza mtaji kwa kuongeza vitendea kazi ambapo tumeweza kununua cherehani ya milioni moja na nusu na kitendea kazi hicho kilitufanya kuwa na kazi kubwa na kwakuwa tumejikita kwenye kutengeneza nguo za wanafunzi. Ameeleza Bi Pole
Veronica Mtilo ambae ni Mwenyekiti wa kikundi cha walemavu Maendeleo Nyakato, alisema kuwa kupitia mkopo huu wameweza kununua mashine kubwa ya kushona masweta yenye thamani ya Shilingi Milioni saba hii ni baada ya kumaliza kulipa mkopo wa awamu ya kwanza huku wakiiomba serikali iendelee kuwasaidia watu wenye ulamavu maana wameweza kuwa na shughuli za kufanya na kuaacha kuomba omba, na alitoa wito kwa walemavu wenzao ambao bado hawajafunguka kuweza kuunda vikundi na wachangamkie fursa hii ili wanufaike na mkopo ambao hauna riba.
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana kupitia mikopo hii zipo changamoto mbalimbali ambazo Halmashauri imekuwa zikikabiliana nazo katika suala hili la utoaji wa mikopo ambazo ni pamoja na baadhi ya vikundi kutokurejesha mkopo kwa wakati, vikundi vingi vya vijana vinavyopata mkopo huu husambaratika hivyo kupelekea kutokurejesha mkopo. Kwa upande wa vikundi vya walemavu wamekuwa wakidhani mkopo huu ni ruzuku hivyo hawarejeshi kabisa au hurejesha kwa kusuasua hivyo.Vikundi vingine hubadili matumizi ya mikopo tofautio na miradi waliyoombea hivyo kupelekea kutofikia malengo yaliyotarajiwa.
Ili kuweza kukabiliana na changamoto hizo, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imejiwekea mikakati mbali ya kuhakikisha kuwa fedha hizi zinaendelea kuwanufaisha makundi haya na kuweza kujikwamua kiuchumi baadhi ya mikakati hiyo ikiwemo ni ufuatiliaji wa marejesho ambapo ipo timu maalum ya ufuatiliaji inayohusisha wataalam wa maendeleo pamoja na madiwani wa viti maalum ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwapa elimu ya urejeshaji wa mikopo.
Ipo mikakati mbalimbali ambayo imewekwa katika kuhakikisha kuwa makundi haya yanawezeshwa na kujikwamua na suala zima la umaskini ikiwemo kuhakikisha kuwa makundi haya yanapewa mkopo mkubwa katika kila kata ambao utawawezesha kutekeleza mradi mkubwa ambao utakuwa wa mfano kwa jamii, pia kuendelea kutoa mikopo midogo midogo kwa makundi hayo.
Mikakati mingine ni pamoja na kuwa Halmashauri imejipanga kutenga eneo kwa ajili ya kuwawezesha vijana kutekeleza shughuli zao za kiuchumi ili kuweza kujikwamu na suala la umaskini, pia ni kuendelea kuhamasisha vikundi hivyo juu ya kuwa na miradi iliyo kwenye muundo wa viwanda.
Katika kipindi cha miaka mitano yaani kuanzia 2015 hadi 2020 jumla ya Shilingi 1,431,000,000 zimetolewa kwa vikundi 414 vya wanawake, vikundi 112 vya vijana na vikundi 13 vya walemavu ambapo wao walihudumiwa ndani ya kipindi cha miaka miwili.
Kwa mwaka wa fedha 2019/2020 asilimia 10 ya fedha iliyotolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu katika Manispaa ya Ilemela ilikuwa ni Shilingi 540,000,000 tu ambapo jumla ya vikundi 166 vya wanawake, vijana na walemavu vilipatiwa mikopo ikiwa vikundi 126 vya wanawake vilipatiwa kiasi cha Shilingi 418,000,000 vikundi 32 vya vijana vilipatiwa shilingi 101,000,000.00 na Shilingi Milioni 21,000,000 ilitolewa kwa vikundi 8 vya walemavu
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.