Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kupitia mapato yake ya ndani imetenga bajeti ya jumla ya kiasi cha shilingi millioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya ndani ya kata ya Ibungilo mtaa wa Kiloleli A ikiwa ni katika jitihada za kupunguza adha inayowakabili wananchi wa eneo hilo kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo ndani ya kata hiyo mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe.Angeline Mabula amesema Manispaa ya Ilemela imeamua kufikia uamuzi wa kubuni miradi mikubwa kwa kutumia fedha za mapato ya ndani kwa kuwa fedha nyingi za mapato ya ndani zimekuwa zikitumika kwa shughuli mbalimbali za kimaendeleo kwa mgawanyo mdogo mdogo.
“ Tumeamua kutenga fedha nyingi za mapato yetu ya Manispaa kwa ajili ya miradi mikubwa ya kuonekana,kata ya Ibungilo ina zaidi ya wakazi 24,000 na haijawahi kuwa na kituo cha afya.Nafikiri ni wakati sasa wa wananchi hawa kusogezewa huduma hizo.”
Aidha Mhe.Mabula ametoa rai kwa wananchi wa kata ya Ibungilo kutoa ushirikiano wa kutosha pindi kazi ya ujenzi itakapoanza na kuwataka kuvaa umiliki wa mali zote zitakazokuwepo kwenye eneo la ujenzi ili kuruhusu kazi iende kwa kasi na mradi kukamilika kwa wakati kwa ajili yao huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa fedha nyingi ndani ya jimbo lake la Ilemela kwa ajili kuchochea shughuli za maendeleo kwa wananchi.
Nae diwani wa kata hiyo Mhe.Hussein Magela amemshukuru Mbunge wa jimbo la Ilemela kwa kazi nzuri anayoendelea nayo na kuzidi kuahidi ushirikiano mkubwa katika shughuli za kuleta maendeleo ndani ya kata yake.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Silvester Mrimi amepokea maagizo yote ya Mbunge wa Ilemela na kumhakikishia utekelezaji kwa awamu kwa kuangalia uhitaji sambamba na bajeti iliyopangwa katika shughuli za maendeleo.
Mama Doreen ni muuzaji wa ndizi katika soko la Kiloleli ambako Mhe.Mbunge alipita kuwasalimia wafanyabiashara wadogowadogo yeye anampongeza Mhe.Mabula kwa namna anavyotembelea wananchi maeneo mengi kujua changamoto zao na kuzitolea majibu kwa wakati.
“ Anafanya vizuri sana huyu mama,hajatuangusha kina mama wenzie.”
Mbali na hayo Mhe.Mabula amekabidhi jumla ya mifuko 100 ya saruji yenye thamani ya shilingi milioni 2.4 kwa ajili ya shughuli za ujenzi na ukarabati wa miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya kata hiyo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.