Lengo kubwa la serikali ni kuona wananchi wake wanaboresha hali zao za kiuchumi kuanzia ngazi ya familia na taifa kwa ujumla, katika kutekeleza azma hii halmashauri ya manispaa ya Ilemela tarehe 28 Februari 2025 ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.13 kwa vikundi 60 villivyokidhi vigezo vya wanawake , vijana na watu wenye ulemavu fedha inayotokana na mapato yake ya ndani ya halmashauri.
Akikabidhi mfano wa hundi kwa vikundi hivyo katibu tawala wa Wilaya ya Ilemela wakili Mariam Msengi akimwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe.Hassan Masala amesema mikopo hiyo ilisimamishwa kutolewa kwa muda kufuatia mapungufu kadhaa yaliyojitokeza kipindi cha nyuma hali iliyopelekea serikali kufanya maboresho katika kuhakikisha wananchi wake wanapata kilicho bora na kwa usalama zaidi hivyo kuwataka wanufaika kwenda kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Nitoe rai yangu kwenu mtumie fursa hii vizuri , mmepitishwa kwenye madarasa mengi sana hadi kufikia hatua ya kupatiwa mkopo, basi fedha hizi mkazitumie kama ilivyokusudiwa, serikali inatamani kuona fedha hizi zinawainua kiuchumi, fedha hizi zitumike kuboresha hali zetu za kiuchumi, tutakapowatembelea basi tukute mmenyanyuka kiuchumi hilo ndio lengo la kwanza”, alisema wakili Mariam
Akiwasilisha taarifa ya utoaji wa mikopo hiyo mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Ilemela Bi.Ummy Wayayu amesema kuwa wamezingatia taratibu zote pamoja muongozo wa utoaji wa mkopo unaozingatia uwiano wa 4:4:2 ambapo vikundi 39 vya wanawake vimeidhinishiwa shilingi milioni 618.60, vikundi 17 vya vijana shilingi milioni 492.90 na vikundi 4 vya watu wenye ulemavu waliidhinishiwa shilingi milioni 24,huku akifafanua kuwa vikundi 32 ambavyo vimekidhi vigezo vitapewa awamu inayofuata
Katika nyakati tofauti wawakilishi wa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu Bi Specioza Alex, Ndg. Jackson Kalunga na Ndg. Yohanna wameishukuru serikali kwa kurejesha utoaji wa mikopo hii ya asilimia 10 na kuahidi kwenda kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa na kuirejesha kwa wakati ili na vikundi vingine viweze kunufaika, huku wakiahidi kuwa mabalozi wazuri wa serikali yao
Mhe Renatus Mulunga Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela ameviasa vikundi hivyo juu ya suala la uadilifu na uaminifu na kusema kuwa baadhi ya vikundi vimekuwa vikitumia fedha hizo kinyume na utaratibu akihitimisha kwa kusema kuwa utoaji wa mikopo hii utagusa kata zote 19 na utafanyika kwa awamu.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.