“Ni wakati wa vijana kuamka na kuacha kukaa vijiweni kupoteza muda bila kazi yoyote,zipo fursa nyingi zinazotolewa na Halmashauri ikiwemo mikopo ya asilimia 10 inayojumuisha makundi matatu ambayo ni vijana 4%,wanawake 4% na walemavu 2%.”
Hayo yamesemwa na Afisa uvuvi wa Manispaa ya Ilemela Ivon Maha wakati wa zoezi la uvunaji samaki kwa awamu ya kwanza kwa vikundi vya vijana vya CHAPAKAZI na CATFISH wanaojihusisha na shughuli za uvuvi wa vizimba katika mtaa wa Igalagala ndani ya kata ya Sangabuye.
Maha amesema shughuli hii ya ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba ni mradi wa kiubunifu uliobuniwa na vijana wenyewe na kuungwa mkono na wataalam wa uvuvi wa Manispaa mpaka kufikia hapa huku akiwataka vijana zaidi wajitokeze kufanya kazi za namna hii.
“Vijana mjitokeze kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji nataka niwatie moyo kuwa shughuli za namna za uvuvi zinawezekana mje mpewe mikopo mfanye kazi za namna hii.”Amesema Maha
Aidha Maha amefafanua kuwa vikundi vyote viwili vinafanya kazi katika mtaa wa Igalagala ndani ya kata ya Sangabuye,kila kikundi kina kizimba cha samaki wake ambapo kila kizimba kina takribani ya jumla ya samaki 36,000 ambapo kwa ujumla vikundi hivyo vina jumla ya samaki 72,000.
Nae Afisa vijana wa Manispaa ya Ilemela Bi.Lucy Nicholaus Matemba amesema vikundi hivyo vilipewa jumla ya shilingi za kitanzania 91,880,000 ya asilimia 10 mnamo mwezi Aprili ,2022.
Baraka Buhegu ni mwenyekiti wa kikundi cha CATFISH yeye anatoa shukrani kwa Halmashauri kwa kuwaamini na kutoa kiasi hicho cha fedha kwa wao kufanya ufugaji wa vizimba vya samaki.
“Leo tunavuna samaki 3,000 ambao tunatarajia kuuza shilingi 5,000 kwa kila samaki matarajio yetu ni kupata jumla ya shilingi milioni 15 na baadhi ya wateja tayari tunao.Tunazidi kuwakaribisha kununua samaki wetu wa viwango kwani ndo tumeanza uvunaji.”Amesema Baraka.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.