Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe Hassan Masala amewataka waheshimiwa Madiwani kuungana na timu za sensa zilizopo katika kata zao ili kuwezesha kaya nyingi kufikiwa na kuweza kukamilisha zoezi hili la sensa kwa asilimia 100.
Ameyasema hayo wakati akihutubia baraza la Madiwani ambapo alitumia fursa hiyo pia kuwapongeza madiwani kwa namna ambavyo wamehamasisha wananchi katika kata zao huku akiwataka kutokuwaachia kazi hii makarani peke yake, kwani inapaswa ikamilike kwa asilimia 100 kufuatia umuhimu wake.
“Madiwani mkaungane na timu zilizopo katika kata zenu ili kaya nyingi zifikiwe na kuweza kukamilisha idadi tarajiwa kwa kadri ya muda ambao tumepewa nawaomba sana mshiriki kikamilifu kwa kuendelea kuwaelimisha wananchi ambao bado hawajahesabiwa umuhimu wa zoezi hili la sensa”, amesema Mhe. Masala
Ameongeza kusema kuwa Mhe Rais, Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kutoa hamasa toka kuanza kwa zoezi hili hivyo haitapendeza inapofika mwisho kukuta kuwa kuna kaya ambayo haijahesabiwa
Licha ya changamoto chache ambazo makarani wamekutana nazo Mhe. Masala amewashukuru wananchi namna ambavyo wamekuwa wakitoa ushirikiano mkubwa na kufikia hatua wananchi hao kuwatafuta makarani wakahesabiwe hii ni dalili kuwa wananchi wameelewa umuhimu wa sensa.
Nae Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mhe.Renatus Mulunga amewataka wananchi kubeba umiliki wa zoezi la sensa ya watu na makazi na kila mmoja kuwa balozi wa mwingine katika kuhamasishana kushiriki kuhesabiwa.
Kaya 41,980 ambayo ni sawa na asilimia 35 zimehesabiwa ndani ya siku mbili toka zoezi la sensa ya watu na makazi kuanza tarehe 23 Agosti 2022, ambapo jumla ya kaya 121,542 zinatarajiwa kuhesabiwa katika Wilaya ya Ilemela, amehitimisha Mhe. Hassan Masala
“ Tushiriki kuhesabiwa kwa maendeleo endelevu.”
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.