Mhe Hasan Masala, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela amesisitiza suala la uadilifu katika mradi wa ujenzi wa kituo cha afya cha Kayenze. Hayo ameyasema wakati wa kuchimba msingi wa kituo hicho ikiwa ni ishara ya kuzindua rasmi ujenzi wa kituo cha afya cha Kayenze.
“Nisistize kama kiongozi wa serikali, uadilifu katika utekelezaji wa mradi huu, kwani fedha hii inatazamwa na wengi, mtu asijaribu kupata kishawishi atakaejaribu kufanya yale ambayo yapo nje ya muongozo wa fedha hii atapata changamoto”.
Aidha Mhe. Masala amezitaka Kamati zikawajibike, kwa kuhakikisha kuwa kumbukumbu zinatunzwa vizuri kuanzia shilingi ya kwanza hadi itapoishia kwani lengo ni kupata zaidi ya majengo matatu na kumaliza mradi kwa ukamilifu wake na ikiwezekana kujenga majengo ya ziada.
Pamoja na maelekezo hayo amewapongeza wananchi kwa utayari wao kuupokea mradi huu, kutoa eneo la ujenzi, na kusema kuwa viongozi watahakikisha kuwa fedha hizi hazitakaa kwenye akaunti na zitafanya kazi iliyokusudiwa ili wananchi waweze kupata majibu ya kero walizokuwa nazo. Huku akiwataka wananchi kumshukuru Mhe. Rais kwa kuleta kiasi cha shilingi 250 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Kayenze.
Nae Diwani wa Kata ya Kayenze,Mhe. Issa Dida amemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuleta fedha za ujenzi wa kituo cha Afya katika kata yake kwani kero ya umbali wa kufuata huduma za afya inaenda kutatuliwa sasa.
Malengo ya ilani ya chama cha mapinduzi ni kutaka kila mwananchi kuwa na afya bora, nguvu ili kuweze kushiriki katika shughuli za ujenzi wa taifa lakini pia kuleta maendeleo katika familia zao. Huku akichambua kwa ufupi Ilani ya CCM upande wa afya kwa kusema kuwa, maandiko ya CCM kwenye ilani ya uchaguzi yanasema kuwa kila palipo na mtaa pawe na zahanati, palipo na kata kuwe na kituo cha afya, na palipo na wilaya iwepo hospitali ya wilaya hayo yamesemwa na katibu wa CCM wa wilaya ya Ilemela Bi Aziza Isimbula.
Nae Mbunge wa jimbo la Ilemela, Mhe. Angeline Mabula ambae alishiriki zoezi hilo la uchimbaji wa msingi, amewaomba wananchi wa kata ya kayenze kuilipa heshima ya kupewa kituo cha afya kayenze kwa kufanya kazi ya mfano na ya viwango isiyokuwa na udokozi huku akitaka kila mtu kuwa mlinzi wa mwenzake,
“Mhe Rais mmemsikia, kuwa ukitaka kumjua rangi zake mchezee pesa, tunachotaka ujenzi wa viwango tushirikiane na kuhakikisha kuwa kazi hii inaenda vizuri”,Alisisitiza
Katika zoezi hilo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary amesema kuwa anatarajia kuwa kazi itaanza mara moja, huku akiwahimiza wakazi wa Kayenze kujitolea kufanya kazi kwani kazi watakayofanya kwa nguvu zao itasaidia kuokoa fedha nyingi, na kuahidi kuchangia matofali elfu kumi katika ujenzi huo.
“Hii kazi ni yenu mjitahidi kutoa nguvu zenu kuchangia ili fedha itakayo okolewa isaidie kujenga jengo jingine”,Alisema.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ilipokea fedha kiasi cha Shilingi Milioni mia mbili na hamsini kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha hicho afya ambapo yatajengwa majengo ya awali ambayo ni jengo la wagonjwa wa nje (OPD),jengo la maabara na kichomea taka.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.