"Tuendelee kufanya hamasa kwa jamii kwani malengo ya serikali ni kuhakikisha kila mtoto anapata chakula shuleni na hii ni agenda ya kudumu"
Ni kauli ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe Hassan Masala wakati wa kikao cha tathmini ya lishe ya wilaya kilichofanyika tarehe 02 Juni 2025 kwa lengo la kujadili taarifa ya robo ya tatu kipindi cha Januari -Machi 2025 .
Aidha Mhe Masala amesisitiza juu ya utoaji wa elimu kwa wazazi kwa kuwaeleza juu ya faida ya watoto wao kupata lishe shuleni ambapo amewahimiza watendaji wa kata kusimamia suala hili.
Sambamba na hilo amewaelekeza Maafisa Elimu Msingi na Sekondari kuwaandikia barua wakuu wa shule na walimu wakuu za kuitisha bodi za shule kwa ajili ya kujadili suala la lishe.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji Bi Pili Kassim ambae ni afisa lishe wa Manispaa ya Ilemela amesema kuwa, katika kipindi cha Januari hadi machi jumla ya shughuli 9 zilitekelezwa hali iliyopelekea kuibua watoto 190 wenye ukondefu, uzito pungufu,udumavu na uzito uliozidi ambapo elimu ya lishe na unasihi wa kilishe ulifanyika katika familia hizo.
Nae Mkurugenzi Ummy Wayayu amemhakikishia Mkuu Wilaya Mhe Masala kuendelea kutoa fedha za lishe kwa ajili ya chakula dawa pamoja na shughuli nyingine za Lishe zinazoendelea kutekelezwa ikiwemo maadhimisho ya siku ya Afya na lishe ya Mtaa.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.